Kum 21:1-9
Kum 21:1-9 SUV
Aonekanapo mtu ameuawa katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, kuimiliki, amelala kondeni, wala haijulikani ni nani aliyempiga; na watoke nje wazee wako na waamuzi wako, nao wapime hapo mpaka miji iliyomzunguka huyo aliyeuawa; na iwe, mji ulio karibu na yule aliyeuawa, wale wazee wake mji huo watwae mtamba katika kundi la ng’ombe, ambaye hajafanya kazi, wala hajakokota jembe la nira; wazee wa mji huo na wamshushe yule mtamba mpaka bonde lenye maji ya mtoni, lisilolimwa wala kupandwa, wakamvunje yule mtamba shingo yake humo bondeni; nao makuhani wana wa Lawi wasongee karibu, kwa kuwa ndio aliowachagua BWANA, Mungu wako, wamtumikie, na kubariki katika jina la BWANA na kila neno lishindaniwalo, na kila pigo, litakuwa kwa kufuata maneno yao; na wazee wote wa mji ule, ulio karibu sana na yule aliyeuawa, na waoshe mikono yao juu ya huyo mtamba aliyevunjwa shingo yake humo bondeni; na wajibizane kwamba, Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuiona. Ee BWANA, samehe watu wako Israeli, uliowakomboa, wala usiache damu ya asiye makosa ikakaa katikati ya watu wako Israeli. Na ile damu utasamehewa kwao. Ndivyo utakavyoondoa damu ya asiye makosa katikati yako, utakapofanya yaliyo sawa machoni pa BWANA.