Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 2

2
Kutangatanga jangwani
1Kisha tukageuka nyuma na kusafiri kuelekea jangwani kwa njia inayoelekea Bahari ya Shamu, kama Mwenyezi Mungu alivyonielekeza. Kwa muda mrefu tulitembea kuzunguka nchi ya vilima ya Seiri.
2Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, 3“Umetembea kuzunguka hii nchi ya vilima kwa muda wa kutosha; sasa geukia kaskazini. 4Wape watu maagizo haya: ‘Mko karibu kupita katikati ya nchi ya ndugu zako ambao ni wazao wa Esau, ambao wanaishi Seiri. Watawaogopa, lakini mwe waangalifu. 5Msiwachokoze kwa vita kwa maana sitawapa ninyi sehemu yoyote ya nchi yao, hata sehemu ya kutosha kuweka wayo wenu juu yake. Nimempa Esau nchi ya vilima ya Seiri kama yake mwenyewe. 6Mtawalipa fedha kwa chakula mtakachokula na maji mtakayokunywa.’ ”
7Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewabariki kwa kazi yote ya mikono yenu. Amewalinda katika safari yenu katikati ya jangwa hili kubwa. Kwa miaka hii arobaini Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amekuwa pamoja nanyi, na hamkupungukiwa na kitu chochote.
8Basi tulipita kwa ndugu zetu wazao wa Esau ambao wanaishi Seiri. Tuligeuka kutoka njia ya Araba ambayo inatokea Elathi na Esion-Geberi, tukasafiri kufuata njia ya jangwa la Moabu.
9Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Usiwasumbue Wamoabu kwa vita, kwa kuwa sitawapa sehemu yoyote ya nchi yao. Nimetoa nchi ya Ari kwa wazao wa Lutu kama milki yao.”
10(Waemi walikuwa wakiishi huko hapo zamani, watu wenye nguvu na wengi, warefu kama Waanaki. 11Kama walivyokuwa Waanaki, hao pia walikuwa kama Warefai, lakini Wamoabu waliwaita Waemi. 12Wahori waliishi Seiri, lakini wazao wa Esau waliwafukuza. Waliwaangamiza Wahori na kukaa mahali pao, kama Waisraeli walivyofanya katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliwapa kama milki yao.)
13Mwenyezi Mungu akasema, “Sasa ondokeni mvuke Bonde la Zeredi.” Hivyo tukavuka bonde.
14Miaka thelathini na nane ilipita tangu wakati tuliondoka Kadesh-Barnea hadi tulipovuka Bonde la Zeredi. Kwa wakati huo kile kizazi chote cha wanaume walioweza kwenda vitani kilikuwa kimekufa, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amewaapia. 15Mkono wa Mwenyezi Mungu uliwakabili hadi alipowaangamiza wote huko kambini.
16Ikawa baada ya mtu wa mwisho wa wale walioweza kwenda vitani kufa, 17Mwenyezi Mungu akaniambia, 18“Leo utapita katika nchi ya Moabu huko Ari. 19Utakapokuja kwa Waamoni, msiwasumbue wala kuwachokoza kwa vita, kwa kuwa sitawapa ardhi yoyote iliyo ya Waamoni kuwa milki yenu. Nimeitoa kama milki ya wazao wa Lutu.”
20(Hiyo pia ilidhaniwa kuwa nchi ya Warefai walioishi huko, lakini Waamoni waliwaita Wazamzumi. 21Walikuwa watu wenye nguvu na wengi, warefu kama Waanaki. Mwenyezi Mungu akawaangamiza kutoka mbele ya Waamoni, ambao waliwafukuza na kukaa mahali pao. 22Mwenyezi Mungu alikuwa amefanya vivyo hivyo kwa wazao wa Esau, ambao waliishi Seiri, alipowaangamiza Wahori watoke mbele yao. Waliwafukuza na wao wakaishi mahali pao hadi leo. 23Nao Waavi ambao waliishi katika vijiji hadi Gaza, Wakaftori waliokuja kutoka Kaftori waliwaangamiza na kukaa mahali pao.)
Kushindwa kwa Sihoni mfalme wa Heshboni
(Hesabu 21:21-30)
24“Ondoka sasa na uvuke Bonde la Arnoni. Tazama, nimemweka mikononi mwako Sihoni Mwamori, mfalme wa Heshboni na nchi yake. Anza kuimiliki nchi hiyo na umwingize katika vita. 25Siku hii ya leo nitaanza kuwatia hofu na woga mataifa yote chini ya mbingu wawaogope ninyi. Watakaposikia taarifa zenu, watatetemeka na kufadhaika kwa sababu yenu.”
26Kutoka jangwa la Kedemothi nilituma wajumbe wenye maneno ya amani kwa Sihoni mfalme wa Heshboni kusema, 27“Turuhusu tupite katika nchi yako. Tutapita katika barabara kuu, hatutageuka kuume wala kushoto. 28Tuuzie chakula tule na maji tunywe kwa thamani yake katika fedha. Turuhusu tu tupite kwa miguu, 29kama wazao wa Esau ambao wanaishi Seiri na Wamoabu ambao wanaishi Ari walivyotufanyia, hadi tuvuke Yordani kuingia nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, anatupatia.” 30Lakini Sihoni mfalme wa Heshboni alikataa kuturuhusu kupita. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alikuwa ameifanya roho yake kuwa ngumu na moyo wake kuwa mkaidi ili amweke kwenye mikono yenu, kama alivyofanya sasa.
31Mwenyezi Mungu akaniambia, “Tazama, nimeanza kuwapa Mfalme Sihoni na nchi yake kwako. Sasa anzeni kuishinda na kuimiliki nchi yake.”
32Sihoni pamoja na jeshi lake lote walipokuja kukutana nasi katika vita huko Yahazi, 33Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alimweka mikononi mwetu, nasi tukamwangamiza pamoja na wanawe na jeshi lake lote. 34Kwa wakati ule tuliteka miji yake yote na kuiangamiza kabisa: wanaume, wanawake na watoto. Hatukumwacha yeyote. 35Lakini mifugo na nyara tulizoziteka kutoka ile miji tulijichukulia wenyewe. 36Kutoka Aroeri kwenye ukingo wa Bonde la Arnoni, kutoka mji ulio ndani ya bonde, hadi kufika Gileadi, hapakuwa na mji hata mmoja uliokuwa na nguvu kutushinda. Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alitupatia yote. 37Lakini kulingana na amri ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, hamkujiingiza katika nchi yoyote ya Waamoni, wala katika sehemu yoyote iliyo kandokando ya Mto Yaboki, wala katika miji iliyo vilimani.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia