Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 1

1
Amri ya kuondoka Mlima Horebu
1Haya ni maneno aliyosema Musa kwa Waisraeli wote jangwani mashariki mwa Yordani, ambayo iko Araba, inayokabiliana na Sufu, kati ya Parani na Tofeli, Labani, Haserothi na Dizahabu. 2(Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya Mlima Seiri hadi Kadesh-Barnea.)
3Katika mwaka wa arobaini, siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na moja, Musa aliwatangazia Waisraeli yale yote Mwenyezi Mungu aliyomwamuru kuwahusu. 4Hii ilikuwa baada ya kumshinda Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala Heshboni, na pia huko Edrei alikuwa amemshinda Ogu mfalme wa Bashani, ambaye alitawala huko Ashtarothi. 5Huko mashariki mwa Yordani katika nchi ya Moabu, Musa alianza kuielezea sheria hii, akisema:
6Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alisema nasi huko Horebu, “Mmekaa muda wa kutosha katika mlima huu. 7Vunjeni kambi, msonge mbele kuelekea nchi ya vilima ya Waamori; nendeni kwa watu wote ambao ni majirani wa Araba, katika milima, Shefela#1:7 au upande wa magharibi chini ya vilima, katika Negebu na kandokando ya pwani, hadi nchi ya Wakanaani na hadi Lebanoni, na kufika mto mkubwa Frati. 8Tazama, nimewapa ninyi nchi hii. Ingieni mkaimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliapa kuwa angewapa baba zenu, Ibrahimu, Isaka na Yakobo, pamoja na uzao wao baada yao.”
Uteuzi wa viongozi
(Kutoka 18:13-27)
9Wakati ule niliwaambia, “Ninyi mmekuwa mzigo mzito sana kwangu kuwachukua peke yangu. 10Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ameongeza hesabu yenu, hivi kwamba leo ninyi ni wengi kama nyota za angani. 11Naye Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, na awaongeze mara elfu na kuwabariki kama alivyoahidi! 12Lakini mimi nitawezaje kubeba matatizo yenu, na mizigo yenu, na magomvi yenu peke yangu? 13Chagueni baadhi ya watu wenye hekima, wenye ufahamu na wanaoheshimika kutoka kila kabila lenu, nami nitawaweka juu yenu.”
14Mlinijibu, “Shauri ulilolitoa ni zuri.”
15Kwa hiyo niliwachukua wanaume viongozi wa makabila yenu, wenye hekima na wanaoheshimika, nami nikawateua wawe na mamlaka juu yenu kama majemadari wa maelfu, wa mamia, wa hamsini, na wa makumi, na kama maafisa wa makabila. 16Nami wakati ule nikawaagiza waamuzi wenu: “Sikilizeni magomvi kati ya ndugu zenu na mwamue kwa haki, hata kama shauri ni kati ya ndugu Waisraeli, au kati ya mmoja wa ndugu Mwisraeli na mgeni. 17Msioneshe upendeleo katika maamuzi; wasikilizeni wote sawasawa, wadogo kwa wakubwa. Msimwogope mtu yeyote, kwa kuwa hukumu ni ya Mungu. Mniletee mimi shauri lolote lililo gumu sana kwenu, nami nitalisikiliza.” 18Nami wakati ule niliwaambia kila kitu ambacho mngefanya.
Wapelelezi wanatumwa
(Hesabu 13:1-33)
19Kisha, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru, tuliondoka kutoka Horebu na kwenda kuelekea nchi ya vilima ya Waamori, kupitia jangwa lile kubwa lote la kutisha, lile mliloliona, nasi tukafika Kadesh-Barnea. 20Kisha niliwaambia, “Mmefika katika nchi ya vilima ya Waamori, ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, anatupatia. 21Tazama, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa nchi. Pandeni mkaimiliki kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, alivyowaambia. Msiogope, wala msikate tamaa.”
22Ndipo ninyi nyote mkanijia na kusema, “Tupeleke watu watutangulie kuipeleleza nchi kwa ajili yetu, na kutuletea taarifa kuhusu njia tutakayopita, na miji tutakayoiendea.”
23Wazo hilo lilionekana zuri kwangu; kwa hiyo niliwachagua watu wenu kumi na wawili, mwanaume mmoja kutoka kila kabila. 24Waliondoka na kukwea katika nchi ya vilima, wakafika katika Bonde la Eshkoli na kuipeleleza. 25Wakachukua baadhi ya matunda ya nchi, wakatuletea na kutuarifu, “Ni nchi nzuri ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, anatupatia.”
Uasi dhidi ya Mwenyezi Mungu
(Hesabu 14:20-45)
26Lakini hamkuwa tayari kukwea, mkaasi dhidi ya amri ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. 27Mkanung’unika ndani ya mahema yenu na kusema, “Mwenyezi Mungu anatuchukia, kwa hiyo alitutoa Misri ili kututia mikononi mwa Waamori kutuangamiza. 28Twende wapi? Ndugu zetu wametufanya kufa moyo. Wanasema, ‘Watu wa huko wana nguvu zaidi na ni warefu kuliko sisi tulivyo; miji ni mikubwa, yenye kuta zilizofika juu angani. Zaidi ya hayo, tumewaona Waanaki huko.’ ”
29Ndipo nikawaambia, “Msihofu, wala msiwaogope. 30Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayewatangulia, atawapigania, kama alivyofanya kwa ajili yenu huko Misri, mbele ya macho yenu hasa, 31na pia huko jangwani. Huko mliona jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowachukua, kama baba amchukuavyo mwanawe, katika njia yote mliyoiendea hadi mkafika mahali hapa.”
32Pamoja na hili, hamkumtegemea Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, 33ambaye aliwatangulia katika safari yenu, kwa moto usiku na kwa wingu mchana, kuwatafutia mahali penu pa kupiga kambi na kuwaonesha njia mtakayoiendea.
34Mwenyezi Mungu aliposikia lile mlilosema, alikasirika, akaapa kwamba: 35“Hakuna mtu wa kizazi hiki kiovu atakayeona nchi nzuri niliyoapa kuwapa baba zenu, 36isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune. Yeye ataiona, nami nitampa yeye na wazao wake nchi aliyoikanyaga kwa miguu, kwa sababu alimfuata Mwenyezi Mungu kwa moyo wote.”
37Kwa sababu yenu Mwenyezi Mungu pia alinikasirikia mimi, akasema, “Hutaingia hiyo nchi pia. 38Lakini msaidizi wako, Yoshua mwana wa Nuni, ataingia. Mtie moyo, kwa sababu atawaongoza Waisraeli kuirithi hiyo nchi. 39Watoto ambao mlisema wangechukuliwa mateka, yaani watoto wenu ambao bado hawajui jema na baya, wataingia katika nchi. Nitawapa hiyo nchi, nao wataimiliki. 40Bali ninyi geukeni, mwondoke kuelekea jangwani kwa kufuata njia ya Bahari ya Shamu.”
41Ndipo mkanijibu, “Tumemtenda Mwenyezi Mungu dhambi. Tutaenda kupigana, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru.” Hivyo kila mmoja wenu akachukua silaha zake, huku mkifikiri kuwa ni rahisi kukwea katika nchi ya vilima.
42Lakini Mwenyezi Mungu aliniambia, “Waambie, ‘Msipande kupigana, kwa sababu sitakuwa pamoja nanyi. Mtashindwa na adui zenu.’ ”
43Hivyo niliwaambia, lakini hamkutaka kusikia. Mliasi dhidi ya amri ya Mwenyezi Mungu, na katika kiburi chenu mlienda katika nchi ya vilima. 44Waamori ambao waliishi katika vilima hivyo waliinuka dhidi yenu, wakawafukuza kama kundi la nyuki wakiwapiga njia yote ya Seiri hadi Horma. 45Mlirudi na kulia mbele za Mwenyezi Mungu, lakini Mungu hakusikiliza kilio chenu, wala hakuwajali. 46Hivyo mlikaa Kadeshi kwa siku nyingi, kwa muda ule wote mliokaa huko.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia