Kumbukumbu 3
3
Kushindwa kwa Ogu mfalme wa Bashani
(Hesabu 21:31-35)
1Kisha tukageuka tukakwea kufuata njia iliyoelekea Bashani, Ogu mfalme wa Bashani akaondoka na jeshi lake lote kupigana na sisi huko Edrei. 2Mwenyezi Mungu akaniambia, “Usimwogope kwa kuwa nimekwisha mkabidhi mikononi mwako pamoja na jeshi lake lote na nchi yake. Umfanyie sawasawa na ulivyomfanyia Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.”
3Hivyo Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, pia akamweka Ogu mfalme wa Bashani pamoja na jeshi lake lote mikononi mwetu. Tuliwaangamiza wote, hakubakia hata mmoja. 4Wakati huo tuliteka miji yake yote. Hakuna mji hata mmoja kati ya ile sitini ambao hatukuuteka, yaani eneo lote la Argobu, utawala wa Mfalme Ogu katika Bashani. 5Miji yote hii ilijengewa ngome zenye kuta ndefu zenye malango na makomeo; pia kulikuwa na vijiji vingi ambavyo havikujengewa kuta. 6Tuliwaangamiza kabisa, kama tulivyomfanyia Sihoni mfalme wa Heshboni, tukiangamiza kila mji, yaani wanaume, wanawake na watoto. 7Lakini wanyama wote wa kufuga pamoja na nyara kutoka miji yao tulichukua vikawa vyetu.
8Hivyo kwa wakati huo tukachukua kutoka kwa wafalme hawa wawili wa Waamori nchi ya mashariki mwa Yordani, kutoka Bonde la Arnoni hadi kufika kwenye Mlima Hermoni. 9(Wasidoni huuita mlima huo Sirioni, nao Waamori huuita Seniri.) 10Tuliteka miji yote kwenye uwanda wa juu, Gileadi yote, Bashani yote hadi Saleka na Edrei, miji ya utawala wa Ogu huko Bashani. 11(Mfalme Ogu wa Bashani ndiye peke yake aliyesalia miongoni mwa mabaki ya Warefai. Kitanda chake kilikuwa cha chuma chenye urefu wa dhiraa tisa#3:11 Dhiraa 9 ni sawa na mita 4. na upana wa dhiraa nne#3:11 Dhiraa 4 ni sawa na mita 1.8.. Hata sasa kinaweza kuonekana katika mji wa Waamoni wa Raba.)
Mgawanyo wa nchi mashariki mwa Yordani
(Hesabu 32:1-42)
12Katika nchi tuliyoiteka wakati ule, niliwapa kabila la Reubeni na Gadi eneo lililoko kaskazini la Aroeri kando ya Bonde la Arnoni, na nusu ya eneo la nchi ya vilima ya Gileadi, pamoja na miji yake. 13Kisha nusu ya kabila la Manase niliwapa sehemu ya Gileadi iliyobaki pamoja na Bashani yote, ambayo ilikuwa utawala wa Ogu. (Eneo lote la Argobu katika Bashani lilikuwa linajulikana kama nchi ya Warefai. 14Yairi, mzao wa kabila la Manase, alichukua eneo lote la nchi ya Argobu hadi kufikia mpaka wa Wageshuri na Wamaaka, ukaitwa kwa jina lake; kwa hiyo hadi leo Bashani inaitwa Hawoth-Yairi.) 15Nikampa Makiri nchi ya Gileadi. 16Lakini niliwapa Wareubeni na Wagadi eneo kuanzia Gileadi hadi Bonde la Arnoni (katikati ya bonde ulikuwa ndio mpaka), kuelekea hadi Mto Yaboki, ambao ndio mpaka wa Waamoni. 17Kwa upande wa magharibi mpaka wao ulikuwa Yordani katika Araba, toka ziwa Galilaya hadi Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), kwenye miteremko ya Pisga upande wa mashariki.
18Wakati huo nilikuamuru: “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekupa nchi hii uimiliki. Lakini ni lazima wanaume wenu wote wenye uwezo, wakiwa wamejiandaa tayari kwa vita, wavuke ng’ambo wakiwatangulia ndugu zako Waisraeli. 19Lakini wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu (kwani najua mnayo mifugo mingi) wanaweza kukaa katika miji niliyowapa, 20hadi hapo Mwenyezi Mungu atakapowapa ndugu zenu kupumzika kama alivyowapa ninyi, wao pia wamiliki ile nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, ng’ambo ya Yordani. Baada ya hapo, kila mmoja wenu anaweza kurudi kwenye milki niliyowapa.”
Musa akatazwa kuvuka Yordani
21Wakati huo nilimwamuru Yoshua, “Umejionea kwa macho yako mwenyewe yale yote ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewafanyia wafalme hawa wawili. Mwenyezi Mungu atazifanyia falme zote huko mnakoenda vivyo hivyo. 22Msiwaogope, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atapigana kwa ajili yenu.”
23Wakati huo nilimsihi Mwenyezi Mungu: 24“Ee Bwana Mungu Mwenyezi, umemwonesha mtumishi wako ukuu wako na mkono wako wenye uweza. Kwa kuwa ni mungu yupi aliye mbinguni au duniani anayeweza kufanya kazi na matendo makuu kama ufanyayo wewe? 25Acha niende nikaione hiyo nchi nzuri ng’ambo ya Yordani, ile nchi nzuri ya vilima na Lebanoni.”
26Lakini kwa sababu yenu Mwenyezi Mungu alinikasirikia na hakutaka kunisikiliza. Mwenyezi Mungu aliniambia, “Hilo latosha; usiseme nami jambo hili tena. 27Kwea juu ya kilele cha Pisga uangalie magharibi, kaskazini, kusini na mashariki. Iangalie hiyo nchi kwa macho yako, kwa vile wewe hutavuka Yordani. 28Lakini mwagize Yoshua, mtie moyo na umtie nguvu, kwa kuwa yeye atawaongoza watu hawa hadi ng’ambo na kuwarithisha nchi utakayoiona.” 29Kwa hiyo tulikaa kwenye bonde karibu na Beth-Peori.
Iliyochaguliwa sasa
Kumbukumbu 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.