Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 16

16
Pasaka
(Kutoka 12:1-20)
1Shikeni mwezi wa Abibu, na kuiadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa sababu katika mwezi wa Abibu, Mungu aliwatoa Misri usiku. 2Mtatoa dhabihu ya Pasaka ya mnyama kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kutoka kundi lenu la mbuzi na kondoo, au la ng’ombe, mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu kuwa makao kwa ajili ya Jina lake. 3Msile nyama hiyo pamoja na mikate iliyotiwa chachu, lakini kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, mikate ya kujitesa, kwa sababu mliondoka Misri kwa haraka, ili siku zote za maisha yenu mpate kukumbuka wakati wenu wa kuondoka Misri. 4Chachu isionekane kwenu katika nchi yenu yote kwa siku saba. Nyama yoyote ya dhabihu mtakayotoa jioni ya siku ya kwanza isibakizwe hadi asubuhi.
5Kamwe msitoe dhabihu ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa, 6isipokuwa mahali atakapopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake. Hapo lazima mtoe dhabihu ya Pasaka jioni jua litakapotua, iwe kumbukumbu yenu ya kutoka Misri. 7Okeni na mle mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kisha asubuhi mrudi kwenye mahema yenu. 8Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu na siku ya saba fanyeni kusanyiko kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na msifanye kazi.
Sikukuu ya Mavuno
(Kutoka 34:22; Walawi 23:15-21)
9Mhesabu majuma saba tangu wakati mnapoanza kuchukua mundu kuvuna nafaka. 10Kisha msherehekee Sikukuu ya Majuma kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari kwa kadiri ya baraka ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa. 11Shangilieni mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua kuwa makao ya Jina lake, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi walio katika miji yenu, na wageni, yatima na wajane wanaoishi miongoni mwenu. 12Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa kule Misri na mfuate amri hizi kwa uangalifu.
Sikukuu ya Vibanda
(Walawi 23:33-43)
13Adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa siku saba baada ya kukusanya mazao kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka, na kutoka shinikizo lako la kukamulia zabibu. 14Mfurahie sikukuu yenu, ninyi, wana wenu, binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu. 15Kwa siku saba mtaiadhimisha sikukuu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, katika mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawabariki katika mavuno yenu na katika kazi zote za mikono yenu na furaha yenu itakamilika.
16Wanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma, na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele za Mwenyezi Mungu mikono mitupu: 17Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowabariki.
Waamuzi
18Wateue waamuzi na maafisa kwa kila kabila lenu katika kila mji ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, nao watawaamua watu kwa usawa. 19Msipotoshe haki wala msifanye upendeleo. Msikubali rushwa kwa sababu rushwa hupofusha macho ya wenye busara na kugeuza maneno ya wenye haki. 20Mfuate haki na haki peke yake, ili mweze kuishi na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa.
Kuabudu miungu mingine
21Msisimamishe nguzo yoyote ya Ashera kando ya madhabahu mliyomjengea Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, 22wala msisimamishe jiwe la kuabudu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anavichukia vitu hivi.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 16: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia