Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 17

17
1Msimtolee Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, dhabihu ya maksai au kondoo aliye na dosari yoyote au hitilafu ndani yake, kwa kuwa hilo litakuwa chukizo kwake.
2Ikiwa mwanaume au mwanamke anayeishi kati ya mojawapo ya miji anayokupa Mwenyezi Mungu, anakutwa anafanya uovu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa kuvunja agano lake, 3naye ameenda kinyume na agizo langu kuabudu miungu mingine na kuisujudia, kama vile jua, mwezi au nyota za angani, 4hili likiwa limeletwa mbele yenu, ni lazima kulichunguza kikamilifu. Ikiwa ni kweli na kuwa limehakikishwa kwamba hili ni chukizo lililofanyika katika Israeli, 5mchukueni huyo mwanaume au mwanamke ambaye amelifanya tendo hili ovu kwenye lango la mji wenu na kumpiga mawe mtu huyo hadi afe. 6Kwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu mtu huyo atauawa, bali hakuna mtu atakayeuawa kwa ushuhuda wa shahidi mmoja tu. 7Ni lazima kwanza mikono ya mashahidi itangulie kumuua huyo mtu, kisha mikono ya watu wote. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.
Mahakama za Sheria
8Kama mashauri yanaletwa katika mahakama zenu ambayo ni magumu zaidi kwenu kuyaamua, ikiwa ni umwagaji wa damu, madai au mashambulio, yapelekeni mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapopachagua. 9Nendeni kwa makuhani, ambao ni Walawi, na kwa mwamuzi ambaye atakuwa kazini wakati huo. Ulizeni kwao nao watawapa maamuzi. 10Ni lazima mtende sawasawa na maamuzi watakayowapa mahali Mwenyezi Mungu atakapopachagua. Kuweni waangalifu kufanya kila kitu watakachowaongoza kufanya. 11Fanyeni sawasawa na sheria wanayowafundisha na maamuzi wanayowapa. Msigeuke mkono wa kuume au kushoto kuacha kufanya yale wanayowaambia. 12Mwanaume atakayeonesha dharau kwa mwamuzi au kwa kuhani ambaye amewekwa kumtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, lazima auawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli. 13Watu wote watasikia na kuogopa, nao hawatakuwa wenye kudharau tena.
Mfalme
14Utakapoingia katika nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kuimiliki na kukaa humo, nanyi mkasema, “Na tumweke mfalme juu yetu kama mataifa yanayotuzunguka,” 15kuweni na uhakika wa kumweka mfalme juu yenu ambaye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atamchagua. Ni lazima atoke miongoni mwa ndugu zenu wenyewe. Msimweke mgeni juu yenu ambaye si ndugu Mwisraeli. 16Hata hivyo, kamwe mfalme asijipatie hesabu kubwa ya farasi kwa ajili yake mwenyewe, au kuwafanya watu warudi Misri ili kupata farasi wengi, kwa maana Mwenyezi Mungu amekuambia, “Hamtairudia njia ile tena.” 17Kamwe asioe wake wengi, la sivyo moyo wake utapotoka. Kamwe asijilimbikizie kiasi kikubwa cha fedha na dhahabu.
18Atakapokuwa amekalia kiti cha ufalme wake, ajiandikie kwenye kitabu nakala ya sheria kwa ajili yake mwenyewe kutoka zile sheria za makuhani ambao ni Walawi. 19Atakuwa na nakala hiyo, naye ataisoma siku zote za maisha yake ili ajifunze kumheshimu Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na kufuata kwa uangalifu maneno yote ya sheria hii na amri hizi, 20naye asijione kuwa ni bora kuliko ndugu zake na kuipotosha sheria. Ndipo yeye na wazao wake watatawala katika ufalme wake kwa muda mrefu katika Israeli.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 17: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia