Kumbukumbu 15
15
Mwaka wa kufuta madeni
(Walawi 25:1-7)
1Kila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni. 2Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa Mwenyezi Mungu wa kufuta madeni umetangazwa. 3Unaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako. 4Hata hivyo, hapatakuwa na maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, 5ikiwa tutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo. 6Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi.
7Ikiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. 8Bali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. 9Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Mwenyezi Mungu dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. 10Mpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. 11Siku zote watakuwa watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe wakarimu kwa ndugu zenu walio maskini na wahitaji katika nchi yenu.
Kuwaacha huru watumwa
(Kutoka 21:1-18)
12Kama Mwebrania mwenzako, mwanaume au mwanamke, akijiuza kwako na kukutumikia miaka sita, katika mwaka wa saba ni lazima umwache aende zake akiwa huru. 13Nawe wakati utakapomwachia usimwache aende mikono mitupu. 14Mpe kwa hiari kutoka kundi lako la kondoo na mbuzi, kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka, na kutoka shinikizo lako la kukamulia zabibu. Mpe kama vile Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alivyokubariki. 15Kumbukeni kuwa ninyi mlikuwa watumwa huko Misri naye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliwakomboa. Ndiyo sababu nimewapa agizo hili leo.
16Lakini mtumishi wako akikuambia, “Sitaki kukuacha,” kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako naye anaridhika nawe, 17ndipo utachukua chuma kidogo utoboe sikio lake hadi hicho chuma kiingie kwenye ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako wa maisha. Ufanye vivyo hivyo kwa mjakazi wako.
18Usifikiri kuwa kuna ugumu kumwacha mtumishi wako huru, kwa sababu utumishi wake kwako kwa miaka hii sita umekuwa wa thamani mara mbili ya ujira wa mtumishi wa kuajiriwa. Naye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakubariki kwa kila kitu utakachofanya.
Wazaliwa wa kwanza wa wanyama
19Wekeni wakfu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa makundi yenu ya ng’ombe na ya mbuzi na kondoo. Maksai walio wazaliwa wa kwanza msiwafanyize kazi, wala msinyoe manyoya ya wazaliwa wa kwanza wa kondoo. 20Kila mwaka ninyi na jamaa zenu mtapaswa kuwala mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, pale mahali atakapopachagua. 21Kama mnyama ana dosari, akiwa ni kilema au kipofu au kama ana kilema kibaya, kamwe usimtoe dhabihu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. 22Itawapasa kumla ninyi wenyewe katika miji yenu. Wote walio najisi na waliotakasika mwaweza kula kama vile mnavyokula paa au kulungu. 23Lakini kamwe msile damu; imwageni ardhini kama maji.
Iliyochaguliwa sasa
Kumbukumbu 15: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.