Danieli 4:18-27
Danieli 4:18-27 NENO
“Hii ndiyo ndoto niliyoipata mimi, Mfalme Nebukadneza. Sasa Belteshaza, niambie maana yake, kwa maana hakuna hata mmoja wa wenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunifasiria. Bali wewe unaweza, kwa sababu roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako.” Ndipo Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza) alipofadhaika sana kwa muda, nayo mawazo yake yakamtia hofu. Basi mfalme akasema, “Belteshaza, usiruhusu ndoto wala maana yake kukutia hofu.” Belteshaza akajibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii ingewahusu adui zako, na maana yake iwahusu watesi wako! Mti uliouona, uliokua ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga na kuonekana duniani kote, ukiwa na majani ya kupendeza na matunda mengi, ukitoa chakula kwa wote, na ukiwapa hifadhi wanyama wa kondeni, na kuwa mahali pa viota katika matawi yake kwa ajili ya ndege wa angani: Ee mfalme, wewe ndiwe ule mti! Umekuwa mkubwa na mwenye nguvu; nao ukuu wako umekua hadi kufika juu angani, nayo mamlaka yako yameenea hadi miisho ya dunia. “Ee mfalme, wewe ulimwona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akasema, ‘Ukateni mti na kuuangamiza, lakini kiacheni kisiki kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kwenye majani ya kondeni, wakati mizizi yake inabaki ardhini. Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, mwacheni aishi kama wanyama pori hadi nyakati saba zipite juu yake.’ “Ee mfalme, hii ndiyo tafsiri, na hii ni amri ya Aliye Juu Sana aliyoitoa dhidi ya bwana wangu mfalme: Wewe utafukuzwa mbali na wanadamu, nawe utaishi pamoja na wanyama pori; utakula nyasi kama ng’ombe, na kuloana kwa umande wa mbinguni. Nyakati saba zitapita hadi utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye. Amri ya kuacha kisiki pamoja na mizizi yake inamaanisha kwamba ufalme wako utarejeshwa kwako utakapokubali kwamba Mbingu ndizo hutawala. Kwa hiyo, ee mfalme, uwe radhi kupokea ushauri wangu: Acha dhambi zako kwa kutenda yaliyo haki, ukaache uovu wako na uwe na huruma kwa waliodhulumiwa. Hivyo itawezekana baada ya hayo, mafanikio yako yataendelea.”