Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 4:18-27

Danieli 4:18-27 Biblia Habari Njema (BHN)

“Hii ndiyo ndoto niliyoota mimi Nebukadneza. Sasa, wewe Belteshaza, nieleze maana yake; kwani wenye hekima wote katika ufalme wangu hawawezi kuniambia maana yake; lakini wewe utaweza kwa kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako.” Hapo, Danieli, aliyeitwa pia Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akamwambia, “Belteshaza, ndoto hii, wala maana yake visikufadhaishe!” Belteshaza akamjibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii na maana yake ingewahusu adui zako! Mti uliouona ukiwa mkubwa na wenye nguvu, ambao matawi yake marefu yalifika mbinguni, nao ukionekana kutoka kila mahali duniani, majani yake yakiwa mazuri, na matunda yake mengi ya kulisha viumbe vyote, wanyama wa porini wakipata kivuli chini yake, na ndege wa angani wakikaa katika matawi yake, basi, ni wewe ee mfalme ambaye umekuwa mkubwa na mwenye nguvu. Ukuu wako umefika mpaka mbinguni, na ufalme wako umeenea mpaka miisho ya dunia. Kisha ukaona tena, ee mfalme, Mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni, akaamuru: ‘Ukateni mti huu, mkauangamize. Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini kwenye majani mabichi ya kondeni, kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini kwa miaka saba.’ “Hii basi, bwana wangu, ndiyo maana ya ndoto yako, kadiri ya uamuzi wa Mungu Mkuu juu yako: Wewe utafukuzwa mbali na wanaadamu! Utaishi pamoja na wanyama wa porini, utakula majani kama ng'ombe; utalowa kwa umande wa mbinguni. Utakaa katika hali hiyo kwa miaka saba, na mwishowe utatambua kwamba Mungu Mkuu ndiye mwenye uwezo juu ya falme za wanaadamu, na humpa ufalme mtu yeyote amtakaye. Tena amri ile ya kukiacha kisiki na mizizi ya mti huo ardhini ina maana hii: Wewe utarudishiwa tena ufalme wako hapo utakapotambua kwamba Mungu wa mbinguni ndiye atawalaye. Kwa sababu hiyo, ee mfalme, sikiliza shauri langu. Achana na dhambi zako na maovu yako, utende haki na kuwaonea huruma waliodhulumiwa; huenda muda wako wa fanaka ukarefushwa!”

Shirikisha
Soma Danieli 4

Danieli 4:18-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mimi, Nebukadneza, nimeiona ndoto hii; na wewe, Ee Belteshaza, eleza tafsiri yake, kwa maana wenye hekima wote wa ufalme wangu hawawezi kunijulisha tafsiri yake; bali wewe waweza, maana roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako. Ndipo Danieli, aliyeitwa jina lake Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akajibu akasema, Ee Belteshaza, ndoto ile isikufadhaishe wala tafsiri yake. Belteshaza akajibu, akasema, Bwana wangu, ndoto hii iwapate wao wakuchukiao, na tafsiri yake iwapate adui zako. Ule mti uliouona, uliokua, ukawa na nguvu, urefu wake ukafika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka dunia yote; ambao majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha wote; ambao chini yake wanyama wa mwituni walikaa, na ndege wa angani walikuwa na makao yao katika matawi yake; ni wewe, Ee mfalme, uliyekua, na kupata nguvu; maana ukuu wako umekua na kufika mpaka mbinguni, na mamlaka yako yamefika mpaka mwisho wa dunia. Tena, kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa mwituni, hata nyakati saba zipite juu yake; tafsiri yake ni hii, Ee mfalme, nayo ni amri yake Aliye Juu, iliyomjia bwana wangu, mfalme; ya kuwa utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa mwituni, nawe utalazimishwa kula majani kama ng'ombe, nawe utanyeshewa na umande wa mbinguni, na nyakati saba zitapita juu yako; hata utakapojua ya kuwa Aliye Juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote. Na kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala. Kwa sababu hiyo, Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; uache dhambi zako kwa kutenda haki, uache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za fanaka.

Shirikisha
Soma Danieli 4

Danieli 4:18-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mimi, Nebukadreza, nimeiona ndoto hii; na wewe, Ee Belteshaza, eleza tafsiri yake, kwa maana wenye hekima wote wa ufalme wangu hawawezi kunijulisha tafsiri yake; bali wewe waweza, maana roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako. Ndipo Danieli, aliyeitwa jina lake Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akajibu akasema, Ee Belteshaza, ndoto ile isikufadhaishe wala tafsiri yake. Belteshaza akajibu, akasema, Bwana wangu, ndoto hii iwapate wao wakuchukiao, na tafsiri yake iwapate adui zako. Ule mti uliouona, uliokua, ukawa na nguvu, urefu wake ukafika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka dunia yote; ambao majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha wote; ambao chini yake wanyama wa kondeni walikaa, na ndege wa angani walikuwa na makao yao katika matawi yake; ni wewe, Ee mfalme, uliyekua, na kupata nguvu; maana ukuu wako umekua na kufika mpaka mbinguni, na mamlaka yako yamefika mpaka mwisho wa dunia. Tena, kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa kondeni, hata nyakati saba zipite juu yake; tafsiri yake ni hii, Ee mfalme, nayo ni amri yake Aliye juu, iliyomjia bwana wangu, mfalme; ya kuwa utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni, nawe utalazimishwa kula majani kama ng’ombe, nawe utatiwa maji kwa umande wa mbinguni, na nyakati saba zitapita juu yako; hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote. Na kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala. Kwa sababu hiyo, Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha.

Shirikisha
Soma Danieli 4

Danieli 4:18-27 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

“Hii ndiyo ndoto niliyoipata mimi, Mfalme Nebukadneza. Sasa Belteshaza, niambie maana yake, kwa maana hakuna hata mmoja wa wenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunifasiria. Bali wewe unaweza, kwa sababu roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako.” Ndipo Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza) alipofadhaika sana kwa muda, nayo mawazo yake yakamtia hofu. Basi mfalme akasema, “Belteshaza, usiruhusu ndoto wala maana yake kukutia hofu.” Belteshaza akajibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii ingewahusu adui zako, na maana yake iwahusu watesi wako! Mti uliouona, uliokua ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga na kuonekana duniani kote, ukiwa na majani ya kupendeza na matunda mengi, ukitoa chakula kwa wote, na ukiwapa hifadhi wanyama wa kondeni, na kuwa mahali pa viota katika matawi yake kwa ajili ya ndege wa angani: Ee mfalme, wewe ndiwe ule mti! Umekuwa mkubwa na mwenye nguvu; nao ukuu wako umekua hadi kufika juu angani, nayo mamlaka yako yameenea hadi miisho ya dunia. “Ee mfalme, wewe ulimwona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akasema, ‘Ukateni mti na kuuangamiza, lakini kiacheni kisiki kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kwenye majani ya kondeni, wakati mizizi yake inabaki ardhini. Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, mwacheni aishi kama wanyama pori hadi nyakati saba zipite juu yake.’ “Ee mfalme, hii ndiyo tafsiri, na hii ni amri ya Aliye Juu Sana aliyoitoa dhidi ya bwana wangu mfalme: Wewe utafukuzwa mbali na wanadamu, nawe utaishi pamoja na wanyama pori; utakula nyasi kama ng’ombe, na kuloana kwa umande wa mbinguni. Nyakati saba zitapita hadi utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye. Amri ya kuacha kisiki pamoja na mizizi yake inamaanisha kwamba ufalme wako utarejeshwa kwako utakapokubali kwamba Mbingu ndizo hutawala. Kwa hiyo, ee mfalme, uwe radhi kupokea ushauri wangu: Acha dhambi zako kwa kutenda yaliyo haki, ukaache uovu wako na uwe na huruma kwa waliodhulumiwa. Hivyo itawezekana baada ya hayo, mafanikio yako yataendelea.”

Shirikisha
Soma Danieli 4