Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 4

4
Ndoto ya Nebukadneza ya mti
1Mfalme Nebukadneza,
Kwa watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wanaoishi duniani kote:
Mafanikio yawe kwenu sana!
2Ni furaha yangu kuwaambia kuhusu ishara za miujiza na maajabu ambayo Mungu Aliye Juu Sana amenifanyia.
3Ishara zake ni kuu kama nini!
Na maajabu yake yana nguvu kama nini!
Ufalme wake ni ufalme wa milele;
enzi yake hudumu kizazi hadi kizazi.
4Mimi, Nebukadneza, nilikuwa nyumbani katika jumba langu la kifalme, nikiishi kwa raha na mafanikio. 5Niliota ndoto iliyoniogopesha. Nilipokuwa nimelala kitandani mwangu, njozi na maono yaliyopita mawazoni mwangu vilinitisha. 6Hivyo nikaagiza kwamba wenye hekima wote wa Babeli waletwe mbele yangu kunifasiria ndoto yangu. 7Waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi walipokuja, niliwaambia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunifasiria. 8Mwishoni, Danieli alikuja mbele yangu, nikamweleza hiyo ndoto. (Danieli anaitwa Belteshaza, kwa jina la mungu wangu, nayo roho ya miungu mitakatifu inakaa ndani yake.)
9Nikasema, “Belteshaza, mkuu wa waganga, ninajua kuwa roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako, wala hakuna siri iliyo ngumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu, nifasirie. 10Haya ndio maono niliyoona nilipokuwa nimelala kitandani mwangu: Nilitazama, na mbele yangu ulisimama mti katikati ya nchi. Ulikuwa mrefu sana. 11Mti ule ulikua, ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga; ulionekana hadi miisho ya dunia. 12Majani yake yalikuwa ya kupendeza, matunda yake yalikuwa mengi, na juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Chini ya kivuli chake wanyama wa kondeni walipata hifadhi, na ndege wa angani waliishi katika matawi yake. Kila kiumbe kililishwa kutokana na mti huo.
13“Katika maono niliyoyaona nikiwa nimelala kitandani mwangu, nilitazama, na mbele yangu nikaona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni. 14Akaita kwa sauti kubwa: ‘Kateni mti huu, myafyeke matawi yake; yaondoeni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na wakimbie kutoka chini yake, na ndege waondoke kutoka matawi yake. 15Lakini kiacheni kisiki na mizizi yake, kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kibaki ardhini, kwenye majani ya kondeni.
“ ‘Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, naye aachwe aishi pamoja na wanyama miongoni mwa mimea ya dunia. 16Akili yake na ibadilishwe kutoka ile ya mwanadamu, na apewe akili ya mnyama, hadi nyakati saba zipite juu yake.
17“ ‘Uamuzi huu umetangazwa na wajumbe; watakatifu, wametangaza hukumu ili walio hai wajue kuwa Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za dunia, naye humpa amtakaye, na kumtawaza juu yake hata yeye aliye mnyonge sana miongoni mwa wanadamu.’
18“Hii ndiyo ndoto niliyoipata mimi, Mfalme Nebukadneza. Sasa Belteshaza, niambie maana yake, kwa maana hakuna hata mmoja wa wenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunifasiria. Bali wewe unaweza, kwa sababu roho ya miungu mitakatifu iko ndani yako.”
Danieli anaifasiri ndoto
19Ndipo Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza) alipofadhaika sana kwa muda, nayo mawazo yake yakamtia hofu. Basi mfalme akasema, “Belteshaza, usiruhusu ndoto wala maana yake kukutia hofu.”
Belteshaza akajibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii ingewahusu adui zako, na maana yake iwahusu watesi wako! 20Mti uliouona, uliokua ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga na kuonekana duniani kote, 21ukiwa na majani ya kupendeza na matunda mengi, ukitoa chakula kwa wote, na ukiwapa hifadhi wanyama wa kondeni, na kuwa mahali pa viota katika matawi yake kwa ajili ya ndege wa angani: 22Ee mfalme, wewe ndiwe ule mti! Umekuwa mkubwa na mwenye nguvu; nao ukuu wako umekua hadi kufika juu angani, nayo mamlaka yako yameenea hadi miisho ya dunia.
23“Ee mfalme, wewe ulimwona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akasema, ‘Ukateni mti na kuuangamiza, lakini kiacheni kisiki kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kwenye majani ya kondeni, wakati mizizi yake inabaki ardhini. Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, mwacheni aishi kama wanyama pori hadi nyakati saba zipite juu yake.’
24“Ee mfalme, hii ndiyo tafsiri, na hii ni amri ya Aliye Juu Sana aliyoitoa dhidi ya bwana wangu mfalme: 25Wewe utafukuzwa mbali na wanadamu, nawe utaishi pamoja na wanyama pori; utakula nyasi kama ng’ombe, na kuloana kwa umande wa mbinguni. Nyakati saba zitapita hadi utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye. 26Amri ya kuacha kisiki pamoja na mizizi yake inamaanisha kwamba ufalme wako utarejeshwa kwako utakapokubali kwamba Mbingu ndizo hutawala. 27Kwa hiyo, ee mfalme, uwe radhi kupokea ushauri wangu: Acha dhambi zako kwa kutenda yaliyo haki, ukaache uovu wako na uwe na huruma kwa waliodhulumiwa. Hivyo itawezekana baada ya hayo, mafanikio yako yataendelea.”
Ndoto inatimia
28Haya yote yalimpata Mfalme Nebukadneza. 29Miezi kumi na mbili baadaye, mfalme alipokuwa akitembea juu ya paa la jumba la kifalme la Babeli, 30alisema, “Je, huu si Babeli mji mkuu nilioujenga uwe makao ya kifalme, kwa uwezo wangu mkubwa, na kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?”
31Maneno hayo yalikuwa bado katika midomo yake wakati sauti ilipokuja kutoka mbinguni, ikisema, “Mfalme Nebukadneza, hiki ndicho kilichoamriwa kwa ajili yako: Mamlaka yako ya ufalme yameondolewa kwako. 32Utafukuzwa mbali na wanadamu, ukaishi pamoja na wanyama pori, na utakula nyasi kama ng’ombe. Nyakati saba zitapita juu yako, hadi utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala katika falme zote za wanadamu, naye humtawaza yeyote amtakaye.”
33Papo hapo yale yaliyokuwa yamesemwa kuhusu Nebukadneza yakatimia. Alifukuzwa mbali na wanadamu, akala nyasi kama ng’ombe. Mwili wake uliloweshwa kwa umande wa mbinguni, hadi nywele zake zikakua kama manyoya ya tai, nazo kucha zake kama makucha ya ndege.
34Mwisho wa wakati huo, mimi Nebukadneza niliinua macho yangu kuelekea mbinguni, nazo fahamu zangu zikanirudia. Ndipo nikamsifu Yeye Aliye Juu Sana, nikamheshimu na kumhimidi yeye aishiye milele.
Utawala wake ni utawala wa milele;
ufalme wake hudumu kizazi hadi kizazi.
35Mataifa yote ya dunia
yanahesabiwa kuwa si kitu.
Hufanya kama atakavyo
kwa majeshi ya mbinguni,
na kwa mataifa ya dunia.
Hakuna anayeweza kuuzuia mkono wake
au kumwambia, “Umefanya nini wewe?”
36Wakati huo huo fahamu zangu ziliponirudia, nikarudishiwa heshima yangu na fahari yangu kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu. Washauri wangu na wakuu wangu walikuja kunitafuta, nami nikarudishwa kwenye kiti changu cha ufalme, hata nikawa mkuu kuliko mwanzoni. 37Basi mimi, Nebukadneza, humhimidi, na humtukuza na kumsifu Mfalme wa mbinguni, kwa sababu kila kitu anachofanya ni haki, na njia zake zote ni adili. Nao wanaoenda kwa kiburi anaweza kuwashusha.

Iliyochaguliwa sasa

Danieli 4: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia