Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 5

5
Maandishi ukutani
1Mfalme Belshaza aliandaa karamu kubwa kwa ajili ya wakuu wake elfu moja, na akanywa mvinyo pamoja nao. 2Belshaza alipokuwa akinywa divai, aliamuru vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekalu huko Yerusalemu viletwe, ili mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wapate kuvinywea. 3Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wakavinywea. 4Walipokuwa wakinywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, ya shaba, chuma, miti na mawe.
5Ghafula vidole vya mkono wa mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya chokaa ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika. 6Uso wa mfalme ukageuka rangi, naye akaogopa sana, kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea.
7Mfalme akawaita wasihiri, wanajimu na waaguzi waletwe, naye akawaambia hao wenye hekima wa Babeli, “Yeyote asomaye maandishi haya na kuniambia maana yake atavikwa nguo za zambarau, na kuvikwa mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atafanywa mtawala wa cheo cha tatu katika ufalme.”
8Ndipo wenye hekima wote wa mfalme wakaingia, lakini hawakuweza kusoma yale maandishi wala kumwambia mfalme maana yake. 9Basi Mfalme Belshaza akazidi kujawa na hofu, na uso wake ukageuka rangi zaidi. Wakuu wake wakapigwa na bumbuazi.
10Malkia#5:10 au mama malkia au mamaye mfalme aliposikia sauti za mfalme na wakuu wake, alikuja katika ukumbi wa karamu. Akasema, “Ee mfalme, uishi milele! Usishtuke! Usibadilike rangi hivyo! 11Yuko mtu katika ufalme wako mwenye roho ya miungu mitakatifu ndani yake. Wakati wa baba yako, mtu huyo alionekana kuwa na ufahamu, akili na hekima kama ile ya miungu. Mfalme Nebukadneza baba yako, naam, mfalme baba yako, alimweka kuwa mkuu wa waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi. 12Mtu huyu Danieli, ambaye mfalme alimwita Belteshaza, alionekana kuwa na akili nyepesi, maarifa na ufahamu, pia uwezo wa kufasiri ndoto, kueleza mafumbo, na kutatua matatizo magumu. Mwite Danieli, naye atakuambia maana ya haya maandishi.”
13Hivyo Danieli akaletwa mbele ya mfalme, naye mfalme akamuuliza, “Je, wewe ndiwe Danieli, mmoja wa watu wa uhamisho walioletwa na mfalme baba yangu kutoka Yuda? 14Nimesikia kwamba roho ya miungu iko ndani yako, na kwamba una ufahamu, akili na hekima ya pekee. 15Watu wenye hekima na wasihiri waliletwa mbele yangu ili kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, lakini hawakuweza kunifafanulia. 16Basi nimesikia kwamba unaweza kutoa tafsiri na kutatua matatizo magumu. Ikiwa unaweza kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, utavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utafanywa mtawala wa tatu katika ufalme.”
17Ndipo Danieli akamjibu mfalme, “Unaweza kubaki na zawadi zako mwenyewe na kumpa mtu mwingine thawabu zako. Hata hivyo, nitasoma maandishi kwa mfalme na kumwambia maana yake.
18“Ee mfalme, Mungu Aliye Juu Sana alimpa baba yako Nebukadneza utawala, ukuu, utukufu na fahari. 19Kwa sababu ya ukuu aliompa baba yako, watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha walimhofu na kumwogopa. Wale ambao mfalme alitaka kuwaua, aliwaua; wale aliotaka kuwaacha hai, aliwaacha hai; wale aliotaka kuwapandisha cheo, aliwapandisha; aliotaka kuwashusha, aliwashusha. 20Lakini moyo wake ulipokuwa na majivuno na kuwa mgumu kwa kiburi, aliondolewa kutoka kwa kiti chake cha ufalme na kuvuliwa utukufu wake. 21Akafukuzwa mbali na wanadamu na kupewa akili ya mnyama, akaishi pamoja na punda-mwitu; akala majani kama ng’ombe, nao mwili wake ukaloweshwa kwa umande wa mbingu, hadi alipotambua kwamba Mungu Aliye Juu Sana ndiye mtawala katika falme zote za wanadamu, na kwamba humtawaza juu yao yeyote amtakaye.
22“Lakini wewe mwanawe, ee Belshaza, hukujinyenyekeza, ingawa ulifahamu haya yote. 23Badala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, pamoja na wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea divai. Uliisifu miungu ya fedha na dhahabu, ya shaba, chuma, miti na mawe, miungu ambayo haiwezi kuona, au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake. 24Kwa hiyo ameutuma mkono ule ulioandika maneno.
25“Haya ndio maneno yaliyoandikwa:
mene, mene,
tekeli, na peresi
26“Hii ndiyo maana ya maneno haya:
Mene: Mungu amezihesabu siku za utawala wako na kuukomesha.
27Tekeli: Wewe umepimwa katika mizani na kuonekana umepungua.
28Peresi: Ufalme wako umegawanywa na kupewa Wamedi na Waajemi.”
29Kwa amri ya Belshaza, Danieli akavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni, tena akatangazwa kuwa mtawala wa tatu katika ufalme.
30Usiku ule ule, Belshaza mfalme wa Wakaldayo akauawa, 31naye Dario Mmedi akanyakua ufalme akiwa na miaka sitini na mbili.

Iliyochaguliwa sasa

Danieli 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia