Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wakolosai 2

2
1Nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walio Laodikia, na pia kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona mimi binafsi. 2Kusudi langu ni watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu mkamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani Al-Masihi, 3ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa. 4Nawaambia mambo haya ili mtu yeyote asiwadanganye kwa maneno matamu. 5Kwa kuwa ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi uthabiti wa imani yenu katika Al-Masihi ulivyo.
Ukamilifu wa maisha katika Al-Masihi
6Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Al-Masihi Isa kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake, 7mkijikita na kujengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani.
8Chungeni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu, yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Al-Masihi.
9Maana utimilifu wote wa Mungu unakaa ndani ya Al-Masihi katika umbile la mwili wa kibinadamu, 10nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Al-Masihi, aliye mkuu juu ya kila nguvu na kila mamlaka. 11Katika Al-Masihi pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Al-Masihi, 12mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo#2:12 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. Wafuasi wa Isa Al-Masihi pia wanapokea Roho wa Mungu kama dhibitisho ya imani yao., na kufufuliwa pamoja naye kupitia kwa imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.
13Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Al-Masihi. Alitusamehe dhambi zetu zote, 14baada ya kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akaigongelea kwenye msalaba wake. 15Baada ya Mungu kuzivua enzi na mamlaka, aliziaibisha hadharani, akishangilia katika ushindi wa msalaba.
16Basi, mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato. 17Hizi zilikuwa kivuli cha mambo yajayo; lakini uhalisi unapatikana kwa Al-Masihi. 18Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza unyenyekevu wa uongo na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu. 19Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua jinsi Mungu anavyouwezesha.
Maonyo dhidi ya walimu wa uongo
20Kwa kuwa mlikufa pamoja na Al-Masihi, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kana kwamba ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri kama hizi: 21“Msishike! Msionje! Msiguse!”? 22Amri hizi zote mwisho wake ni kuharibika zinapotumiwa, kwa sababu msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu. 23Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hazifai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.

Iliyochaguliwa sasa

Wakolosai 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia