Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wakolosai 1

1
Salamu
1Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa, kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu.
2Kwa ndugu watakatifu na waaminifu katika Al-Masihi wanaoishi Kolosai.
Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba#1:2 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, ziwe nanyi.
Shukrani na maombi
3Siku zote tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi, tunapowaombea ninyi, 4kwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Al-Masihi Isa, na upendo wenu mlio nao kwa watakatifu wote: 5imani na upendo ule unaotoka katika tumaini mlilowekewa akiba mbinguni, na ambalo mmesikia habari zake katika neno la kweli, yaani ile Injili 6iliyowafikia ninyi. Duniani kote Injili hii inazaa matunda na kuenea kama ilivyokuwa kwenu tangu siku ile mlipoisikia na kuielewa neema ya Mungu katika kweli yote. 7Mlijifunza habari zake kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu mpendwa, aliye mhudumu mwaminifu wa Al-Masihi kwa ajili yenu, 8ambaye pia ametuambia kuhusu upendo wenu katika Roho wa Mungu.
9Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana Isa, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, 11mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha 12mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake Mpendwa, 14ambaye kwake tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.
Ukuu wa Al-Masihi
15Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16Kwake yeye vitu vyote vilivyo mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya utawala au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa kupitia kwake na kwa ajili yake. 17Yeye alikuwako kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani jumuiya ya waumini, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. 19Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake, 20na kupitia kwake aweze kuvipatanisha vitu vyote kwake mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake iliyomwagika msalabani.
21Hapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya. 22Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kupitia kwa mwili wa Al-Masihi kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama, 23ikiwa mnaendelea katika imani yenu mkiwa imara na thabiti, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa katika Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia, ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu, na ambayo mimi Paulo nimekuwa mtumwa wake.
Taabu ya Paulo kwa ajili ya waumini
24Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Al-Masihi kwa ajili ya mwili wake, ambao ni jumuiya ya waumini. 25Mimi nimekuwa mtumishi wa jumuiya ya waumini kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi neno la Mungu kwa ukamilifu: 26Hii ni siri iliyokuwa imefichika tangu zamani na kwa vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu. 27Kwao Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu wa Mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Al-Masihi ndani yenu, tumaini la utukufu.
28Yeye ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Al-Masihi. 29Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zake ambazo hutenda kazi ndani yangu kwa uweza mwingi.

Iliyochaguliwa sasa

Wakolosai 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia