Wakolosai 2:16-23
Wakolosai 2:16-23 NENO
Basi, mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato. Hizi zilikuwa kivuli cha mambo yajayo; lakini uhalisi unapatikana kwa Al-Masihi. Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza unyenyekevu wa uongo na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu. Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua jinsi Mungu anavyouwezesha. Kwa kuwa mlikufa pamoja na Al-Masihi, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kana kwamba ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri kama hizi: “Msishike! Msionje! Msiguse!”? Amri hizi zote mwisho wake ni kuharibika zinapotumiwa, kwa sababu msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu. Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hazifai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.