Wakolosai 2:16-23
Wakolosai 2:16-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo, basi, msikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu vyakula au vinywaji, siku za sherehe, sikukuu ya mwezi mpya au Sabato. Mambo ya aina hiyo ni kivuli tu cha yale yatakayokuja; ukweli wenyewe ndiye Kristo. Msikubali kuhukumiwa na mtu yeyote anayejitakia kuwa wa maana kwa sababu ya maono ya pekee na ambaye anasisitiza juu ya unyenyekevu wa uongo na ibada kwa malaika. Mtu wa namna hiyo amepumbazika kwa fikira danganyifu za kidunia na amejitenga na Kristo aliye kichwa cha huo mwili. Chini ya uongozi wa Kristo, mwili wote unalishwa na kuunganishwa pamoja kwa viungo na mishipa yake, nao hukua kama atakavyo Mungu. Nyinyi mmekufa pamoja na Kristo na kukombolewa katika nguvu za pepo watawala wa ulimwengu. Kwa nini, basi, kuishi tena kama vile mngekuwa wa ulimwengu huu? Ya nini kuwekewa masharti: “Msishike hiki,” “Msionje kile,” “Msiguse kile!” Mambo hayo yote yanahusika na vitu vyenye kuharibika mara tu vinapotumiwa; hayo ni maagizo na mafundisho ya kibinadamu tu. Kweli, masharti hayo yaonekana kuwa ya hekima kwa namna ya ibada wanayojishurutishia, unyenyekevu, na kuutendea mwili kwa ukali; lakini hayafai chochote kuzuia tamaa za mwili.
Wakolosai 2:16-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. Mtu asiwanyang'anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili; wala hakishiki Kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukineemeshwa na kuungamanishwa kwa viungo na mishipa, hukua kama atakavyo Mungu. Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani, Msishike, msionje, msiguse; (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu? Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.
Wakolosai 2:16-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili; wala hakishiki Kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na kuungamanishwa kwa viungo na mishipa, hukua kwa maongeo yatokayo kwa Mungu. Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani, Msishike, msionje, msiguse; (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu? Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.
Wakolosai 2:16-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato. Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo. Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kunyenyekea kwake na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu. Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu. Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri: “Msishike! Msionje! Msiguse!”? Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu. Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.