Matendo 10:23-33
Matendo 10:23-33 NENO
Basi Petro akawakaribisha ndani wawe wageni wake. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye. Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa na rafiki zake wa karibu. Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni mwake kwa heshima. Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.” Petro alipokuwa akizungumza naye, akaingia ndani na kuwakuta watu wengi wamekusanyika. Akawaambia, “Mnajua kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi. Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?” Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizong’aa akasimama mbele yangu, akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na misaada yako kwa maskini imekumbukwa mbele za Mungu. Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’ Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”