Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 10:23-33

Matendo 10:23-33 SRUV

Akawakaribisha wawe wageni wake. Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye. Kesho yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, akiwa amekusanya jamaa zake na rafiki zake. Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguuni mwake, akamsujudia. Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu. Na katika kusema naye akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika. Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali kwa mtu aliye Myahudi ashirikiane na mtu wa taifa lingine wala kumtembelea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu yeyote mchafu wala najisi. Kwa sababu hiyo nilikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani mliloniitia? Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, akiwa amevaa nguo zinazong'aa, akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu. Basi, tuma watu kwenda Yafa, ukamwite Simoni aitwaye Petro, anakaa katika nyumba ya Simoni, mtengenezaji wa ngozi, karibu na pwani; naye akija atasema nawe. Mara nikatuma watu kwako, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tupo hapa mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana.

Soma Matendo 10