Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 10

10
Kornelio amwita Petro
1Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu aliyeitwa Kornelio, aliyekuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. 2Yeye na jamaa yake yote walikuwa wacha Mungu; alitoa kwa ukarimu kwa wale walio na mahitaji na kumwomba Mungu mara kwa mara. 3Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!”
4Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?”
Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. 5Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro. 6Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”
7Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia. 8Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.
Maono ya Petro
9Siku iliyofuata, walipokuwa wanaukaribia mji, yapata saa sita mchana, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. 10Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. 11Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama kitambaa kikubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. 12Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. 13Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”
14Petro akajibu, “La hasha, Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”
15Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”
16Jambo hili lilitokea mara tatu, na ghafula kile kitambaa kikarudishwa mbinguni.
17Petro alipokuwa akisumbuka kuhusu maana ya maono hayo, wale watu waliotumwa na Kornelio waliipata nyumba ya Simoni, wakasimama kwenye lango. 18Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.
19Wakati Petro akiwa anafikiria kuhusu yale maono, Roho wa Mungu akamwambia, “Simoni, kuna watu watatu wanaokutafuta. 20Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”
21Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”
22Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani mwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” 23Basi Petro akawakaribisha ndani wawe wageni wake. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.
Petro nyumbani mwa Kornelio
24Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa na rafiki zake wa karibu. 25Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni mwake kwa heshima. 26Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”
27Petro alipokuwa akizungumza naye, akaingia ndani na kuwakuta watu wengi wamekusanyika. 28Akawaambia, “Mnajua kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi. 29Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”
30Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizong’aa akasimama mbele yangu, 31akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na misaada yako kwa maskini imekumbukwa mbele za Mungu. 32Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’ 33Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”
Hotuba ya Petro
34Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye. 36Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza Injili ya amani kupitia kwa Isa Al-Masihi. Yeye ni Bwana wa wote. 37Mnajua yale yaliyotukia katika Yudea yote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yahya: 38Jinsi Mungu alivyompaka mafuta Isa Al-Nasiri katika Roho wa Mungu, na jinsi alivyoenda kila mahali akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.
39“Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Yudea na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani. 40Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. 41Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alipakwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu. 43Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”
Watu wa mataifa wapokea Roho wa Mungu
44Petro alipokuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu wa Mungu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45Wale waumini waliokuwa wametahiriwa waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho wa Mungu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa. 46Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.
Ndipo Petro akasema, 47“Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu wa Mungu kama sisi tulivyompokea.” 48Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Isa Al-Masihi. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 10: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia