Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 23:26-37

2 Wafalme 23:26-37 NENO

Hata hivyo, Mwenyezi Mungu hakuacha ghadhabu yake iliyowaka dhidi ya Yuda kwa sababu ya yale yote ambayo Manase alikuwa amefanya kumghadhibisha. Hivyo Mwenyezi Mungu akasema, “Nitamwondoa Yuda mbele zangu kama nilivyomwondoa Israeli, nami nitaukataa Yerusalemu, mji niliouchagua, na Hekalu hili, ambalo nilisema, ‘Jina langu litakaa humo.’” Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yosia na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Yosia alipokuwa mfalme, Farao Neko mfalme wa Misri akapanda hadi Mto Frati kumsaidia mfalme wa Ashuru. Mfalme Yosia akatoka kwenda kupigana naye, lakini Neko akamkabili na kumuua huko Megido. Watumishi wa Yosia wakauleta mwili wake katika gari la vita kutoka Megido hadi Yerusalemu, wakamzika kwenye kaburi lake mwenyewe. Nao watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia, wakampaka mafuta na kumfanya mfalme mahali pa baba yake. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na tatu alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miezi mitatu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia kutoka Libna. Akafanya maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba zake walivyofanya. Farao Neko akamfunga kwa minyororo huko Ribla katika nchi ya Hamathi ili asiweze kutawala huko Yerusalemu, naye akatoza kodi ya talanta mia moja za fedha, na talanta moja ya dhahabu katika Yuda. Farao Neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia, na kulibadilisha jina la Eliakimu kuwa Yehoyakimu. Lakini akamchukua Yehoahazi na kumpeleka Misri, naye akafia huko. Yehoyakimu akamlipa Farao Neko ile fedha na dhahabu aliyodai. Ili kuweza kufanya hivyo, Yehoyakimu akatoza nchi kodi na kulipiza fedha na dhahabu kutoka kwa watu wa nchi kulingana na makadirio ya mapato yao. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Zebida binti Pedaya kutoka Ruma. Naye akafanya maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba zake walivyokuwa wamefanya.