2 Fal 23:26-37
2 Fal 23:26-37 SUV
Walakini BWANA hakuuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, ambayo kwayo hasira yake iliwaka juu ya Yuda, kwa sababu ya machukizo yote ambayo Manase amemchukiza. BWANA akasema Nitawahamisha Yuda pia mbali nami, kama nilivyowahamisha Israeli, nami nitautupa mji huu niliouchagua, naam, Yerusalemu, na nyumba ile niliyoinena, Jina langu litakuwa humo. Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Katika siku zake, Farao-neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana na mfalme wa Ashuru, akafika mto Frati; naye mfalme Yosia akaenda kupigana naye; naye mfalme wa Misri akamwua huko Megido, hapo alipoonana naye. Watumishi wake wakamchukua garini, amekwisha kufa, kutoka Megido, wakamleta Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake mwenyewe. Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta, wakamtawaza awe mfalme badala ya baba yake. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali binti Yeremia wa Libna. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake. Naye Farao-neko akamfunga huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ili asitawale huko Yerusalemu. Akaitoza nchi kodi talanta mia za fedha na talanta ya dhahabu. Farao-neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia awe mfalme mahali pa Yosia babaye, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu, lakini akamwondoa Yehoahazi; akaenda naye Misri, naye akafa huko. Na Yehoyakimu akampa Farao dhahabu na fedha; lakini akaitoza nchi kodi, ili apate kutoa zile fedha kwa amri yake Farao; akawatoza fedha na dhahabu watu wa nchi, kila mtu kwa kodi yake, ili ampe Farao-neko. Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Zebida binti Pedaya wa Ruma. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake.