2 Wafalme 23
23
Yosia analifanya upya agano
(2 Nyakati 34:3-7, 29-33)
1Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. 2Akapanda kwenda hekaluni mwa Mwenyezi Mungu pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, kilichokuwa kimepatikana katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. 3Mfalme akasimama karibu na nguzo, na kufanya upya agano mbele za Mwenyezi Mungu: kwamba atamfuata Mwenyezi Mungu na kuzishika amri zake, maagizo na sheria zake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, na hivyo kuyathibitisha maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika agano.
4Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu hadi Betheli. 5Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani. 6Akaiondoa nguzo ya Ashera kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wasio na cheo. 7Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, nyumba ambazo wanawake walifumia pazia kwa ajili ya Ashera.
8Yosia akawaleta makuhani wote wa Mwenyezi Mungu kutoka miji yote ya Yuda, na kunajisi mahali pa juu pa kuabudia, kuanzia Geba hadi Beer-Sheba, mahali pote ambapo hao makuhani wa miungu walifukiza uvumba. Akabomoa mahali pa kuwekea vitu vya ibada za miungu palipokuwa katika malango, kwenye ingilio la Lango la Yoshua, mtawala wa mji, lililoko upande wa kushoto wa lango la mji. 9Ingawa makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia hawakuhudumu katika madhabahu ya Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu, walikula mikate isiyotiwa chachu pamoja na ndugu zao.
10Kisha mfalme akapanajisi Tofethi, palipokuwa katika Bonde la Ben-Hinomu, ili mtu yeyote asiweze kupatumia kumtoa kafara mwanawe wa kiume au wa kike katika moto kwa Moleki. 11Akaondoa kutoka ingilio la Hekalu la Mwenyezi Mungu wale farasi ambao wafalme wa Yuda walikuwa wamewaweka wakfu kwa ajili ya jua. Walikuwa kwenye ua karibu na chumba cha afisa aliyeitwa Nathan-Meleki. Basi Yosia akayachoma moto yale magari ya vita yaliyokuwa yamewekwa wakfu kwa jua.
12Alizivunja madhabahu ambazo wafalme wa Yuda walikuwa wamezijenga kwenye paa la ghorofa ya Ahazi, pia madhabahu alizokuwa amezijenga Manase katika nyua mbili za Hekalu la Mwenyezi Mungu. Akaziondoa huko, akazivunja vipande vipande, na kutupa hicho kifusi katika Bonde la Kidroni. 13Mfalme pia akanajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, zilizokuwa mashariki mwa Yerusalemu upande wa kusini wa Kilima cha Uharibifu, ambapo Sulemani mfalme wa Israeli alikuwa amejenga mahali pa kuabudia kwa ajili ya Ashtorethi mungu wa kike wa Wasidoni, aliyekuwa chukizo; na kwa ajili ya Kemoshi mungu wa Wamoabu, aliyekuwa chukizo; na kwa ajili ya Moleki mungu wa watu wa Amoni, aliyekuwa chukizo. 14Yosia akapasua yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Ashera. Kisha akafunika hayo maeneo kwa mifupa ya wanadamu.
15Hata madhabahu yaliyokuwa huko Betheli, mahali pa juu pa kuabudia palipokuwa pamejengwa na Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya Israeli watende dhambi, alibomoa hata hayo madhabahu na mahali pa juu pa kuabudia. Alipateketeza kwa moto hapo mahali pa juu pa kuabudia na kupasaga hadi pakawa vumbi, na kuichoma hiyo nguzo ya Ashera pia. 16Kisha Yosia akatazama huku na huko, naye alipoona makaburi yaliyokuwa kwenye kilima, akaamuru mifupa itolewe humo na akaichoma juu ya madhabahu ya Betheli ili kupanajisi. Hili lilitendeka kulingana na neno la Mwenyezi Mungu lililosemwa na mtu wa Mungu ambaye alitangulia kusema mambo haya.
17Mfalme akauliza, “Lile kaburi lenye mnara wa ukumbusho ninaloliona ni kwa ajili gani?”
Watu wa mji wakasema, “Hii ni alama ya kaburi la mtu wa Mungu aliyekuja kutoka Yuda, naye akanena dhidi ya madhabahu ya Betheli mambo yale yale uliyoifanyia leo.”
18Akasema, “Liacheni, msiliguse. Msimruhusu mtu yeyote kuiondoa mifupa yake.” Basi wakaiacha mifupa yake pamoja na ile ya yule nabii aliyekuwa amekuja kutoka Samaria.
19Kama alivyokuwa amefanya huko Betheli, Yosia akabomoa nyumba za ibada katika mahali pa juu pa kuabudia, ambazo wafalme wa Israeli walikuwa wamejenga ndani ya miji ya Samaria, na ambazo zilikuwa zimemghadhibisha Mwenyezi Mungu. 20Yosia akawachinja makuhani wote wa mahali pa juu pa kuabudia katika madhabahu zao wenyewe, na kuchoma mifupa ya wanadamu juu yake. Kisha akarudi Yerusalemu.
Yosia aadhimisha Pasaka
21Mfalme akatoa agizo hili kwa watu wote: “Adhimisheni Pasaka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama ilivyoandikwa katika Kitabu hiki cha Agano.” 22Hapakuwahi kuwa na adhimisho lingine la Pasaka kama hilo tangu nyakati za waamuzi walioamua Israeli, wala katika nyakati zote za wafalme wa Israeli na wafalme wa Yuda. 23Lakini katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia, Pasaka hii iliadhimishwa kwa Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu.
24Zaidi ya hayo, Yosia akawaondoa waaguzi, waabudu mizimu, miungu ya nyumbani, sanamu za kuabudiwa, na vitu vingine vyote vya machukizo vilivyoonekana huko Yuda na Yerusalemu. Aliyafanya haya ili kutimiza matakwa ya sheria iliyoandikwa katika kile kitabu ambacho Hilkia kuhani alikipata ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu. 25Hapakuwepo mfalme mwingine kabla na baada ya Yosia aliyempenda Mwenyezi Mungu kama yeye; kwa moyo wake wote, kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, kulingana na Torati yote ya Musa.
26Hata hivyo, Mwenyezi Mungu hakuacha ghadhabu yake iliyowaka dhidi ya Yuda kwa sababu ya yale yote ambayo Manase alikuwa amefanya kumghadhibisha. 27Hivyo Mwenyezi Mungu akasema, “Nitamwondoa Yuda mbele zangu kama nilivyomwondoa Israeli, nami nitaukataa Yerusalemu, mji niliouchagua, na Hekalu hili, ambalo nilisema, ‘Jina langu litakaa humo.’#23:27 1 Wafalme 8:29”
28Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yosia na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
29Yosia alipokuwa mfalme, Farao Neko mfalme wa Misri akapanda hadi Mto Frati kumsaidia mfalme wa Ashuru. Mfalme Yosia akatoka kwenda kupigana naye, lakini Neko akamkabili na kumuua huko Megido. 30Watumishi wa Yosia wakauleta mwili wake katika gari la vita kutoka Megido hadi Yerusalemu, wakamzika kwenye kaburi lake mwenyewe. Nao watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia, wakampaka mafuta na kumfanya mfalme mahali pa baba yake.
Yehoahazi mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 36:2-4)
31Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na tatu alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miezi mitatu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia kutoka Libna. 32Akafanya maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba zake walivyofanya.
33Farao Neko akamfunga kwa minyororo huko Ribla katika nchi ya Hamathi ili asiweze kutawala huko Yerusalemu, naye akatoza kodi ya talanta mia moja#23:33 Talanta 100 ni sawa na tani 3.4. za fedha, na talanta moja#23:33 Talanta moja ni sawa na kilo 34. ya dhahabu katika Yuda.
Yehoyakimu mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 36:5-8)
34Farao Neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia, na kulibadilisha jina la Eliakimu kuwa Yehoyakimu. Lakini akamchukua Yehoahazi na kumpeleka Misri, naye akafia huko.
35Yehoyakimu akamlipa Farao Neko ile fedha na dhahabu aliyodai. Ili kuweza kufanya hivyo, Yehoyakimu akatoza nchi kodi na kulipiza fedha na dhahabu kutoka kwa watu wa nchi kulingana na makadirio ya mapato yao.
36Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Zebida binti Pedaya kutoka Ruma. 37Naye akafanya maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba zake walivyokuwa wamefanya.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wafalme 23: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.