Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 23:1-14

2 Wafalme 23:1-14 NENO

Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. Akapanda kwenda hekaluni mwa Mwenyezi Mungu pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, kilichokuwa kimepatikana katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Mfalme akasimama karibu na nguzo, na kufanya upya agano mbele za Mwenyezi Mungu: kwamba atamfuata Mwenyezi Mungu na kuzishika amri zake, maagizo na sheria zake kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, na hivyo kuyathibitisha maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika agano. Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu hadi Betheli. Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani. Akaiondoa nguzo ya Ashera kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wasio na cheo. Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, nyumba ambazo wanawake walifumia pazia kwa ajili ya Ashera. Yosia akawaleta makuhani wote wa Mwenyezi Mungu kutoka miji yote ya Yuda, na kunajisi mahali pa juu pa kuabudia, kuanzia Geba hadi Beer-Sheba, mahali pote ambapo hao makuhani wa miungu walifukiza uvumba. Akabomoa mahali pa kuwekea vitu vya ibada za miungu palipokuwa katika malango, kwenye ingilio la Lango la Yoshua, mtawala wa mji, lililoko upande wa kushoto wa lango la mji. Ingawa makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia hawakuhudumu katika madhabahu ya Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu, walikula mikate isiyotiwa chachu pamoja na ndugu zao. Kisha mfalme akapanajisi Tofethi, palipokuwa katika Bonde la Ben-Hinomu, ili mtu yeyote asiweze kupatumia kumtoa kafara mwanawe wa kiume au wa kike katika moto kwa Moleki. Akaondoa kutoka ingilio la Hekalu la Mwenyezi Mungu wale farasi ambao wafalme wa Yuda walikuwa wamewaweka wakfu kwa ajili ya jua. Walikuwa kwenye ua karibu na chumba cha afisa aliyeitwa Nathan-Meleki. Basi Yosia akayachoma moto yale magari ya vita yaliyokuwa yamewekwa wakfu kwa jua. Alizivunja madhabahu ambazo wafalme wa Yuda walikuwa wamezijenga kwenye paa la ghorofa ya Ahazi, pia madhabahu alizokuwa amezijenga Manase katika nyua mbili za Hekalu la Mwenyezi Mungu. Akaziondoa huko, akazivunja vipande vipande, na kutupa hicho kifusi katika Bonde la Kidroni. Mfalme pia akanajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, zilizokuwa mashariki mwa Yerusalemu upande wa kusini wa Kilima cha Uharibifu, ambapo Sulemani mfalme wa Israeli alikuwa amejenga mahali pa kuabudia kwa ajili ya Ashtorethi mungu wa kike wa Wasidoni, aliyekuwa chukizo; na kwa ajili ya Kemoshi mungu wa Wamoabu, aliyekuwa chukizo; na kwa ajili ya Moleki mungu wa watu wa Amoni, aliyekuwa chukizo. Yosia akapasua yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Ashera. Kisha akafunika hayo maeneo kwa mifupa ya wanadamu.