2 Fal 23:1-14
2 Fal 23:1-14 SUV
Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya BWANA. Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile. Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la BWANA vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akavipiga moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli. Akawaondosha wale makuhuni walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni. Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya BWANA, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuiponda-ponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu. Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa BWANA, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera. Akawatoa makuhani wote katika miji ya Yuda, akapanajisi mahali pa juu, makuhani walipokuwa wamefukiza uvumba, tangu Geba hata Beer-sheba; akapavunja mahali pa juu pa malango, palipokuwapo penye kuingia lango la Yoshua, liwali wa mji, palipokuwa upande wa kushoto wa mtu langoni pa mji. Walakini hao makuhani wa mahali pa juu hawakupanda madhabahuni kwa BWANA katika Yerusalemu, bali wakala mikate isiyo na chachu katikati ya ndugu zao. Naye akainajisi Tofethi, iliyomo katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu asipitishe mwana wake au binti yake motoni kwa Moleki. Akawaondoa farasi ambao wafalme wa Yuda waliwatoa kwa jua, hapo pa kuingia nyumbani mwa BWANA, karibu na chumba cha Nathan-Meleki, towashi, kilichohuwako kiungani; akayapiga moto magari ya jua. Nazo madhabahu zilizokuwako darini juu ya chumba cha juu cha Ahazi, wafalme wa Yuda walizozifanya, nazo madhabahu alizozifanya Manase katika behewa mbili za nyumba ya BWANA, mfalme akazivunja, akazitelemsha huko nje, na kuyatupa mavumbi yake katika kijito cha Kidroni. Na mahali pa juu palipokuwapo mbele ya Yerusalemu, palipokuwa upande wa kuume wa mlima wa uharibifu, alipopajenga Sulemani, mfalme wa Israeli, kwa Ashtorethi, chukizo la Wasidoni, na Kemoshi, chukizo la Moabu, na Milkomu, chukizo la wana wa Amoni, mfalme akapanajisi. Akazivunja-vunja nguzo, akayakata-kata maashera, akapajaza mahali pake mifupa ya watu.