Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 17:1-18

2 Wafalme 17:1-18 NENO

Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Ahazi mfalme wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka tisa. Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, lakini si kama wafalme wengine wa Israeli waliomtangulia. Mfalme Shalmanesa wa Ashuru akaenda na kumshambulia Mfalme Hoshea, ambaye hapo awali alikuwa akimlipa ushuru kwa sababu alikuwa mtumishi wake. Lakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri. Wala hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumfunga gerezani. Mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akapigana dhidi ya Samaria na kuuzingira kwa miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaiteka Samaria na kuwahamishia Waisraeli huko Ashuru. Akawakalisha huko Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi. Yote haya yalitukia kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, aliyekuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine, na kufuata desturi za mataifa ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta. Waisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye ngome, walijijengea mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote. Wakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda. Wakafukiza uvumba kila mahali pa juu pa kuabudia, kama yalivyofanya yale mataifa ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha Mwenyezi Mungu. Wakatumikia sanamu, ingawa Mwenyezi Mungu alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.” Mwenyezi Mungu akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Shikeni amri na maagizo yangu, kufuatana na Torati yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii, na ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu, manabii.” Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumwamini Mwenyezi Mungu, Mungu wao. Walizikataa amri zake, na agano alilolifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu batili, nao wenyewe wakawa batili. Wakayaiga mataifa yaliyowazunguka, ingawa Mwenyezi Mungu alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya.” Wakayaacha maagizo yote ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali. Wakawatoa kafara watoto wao wa kiume na wa kike katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa Mwenyezi Mungu, wakamghadhibisha. Basi Mwenyezi Mungu akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki.