Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 17:1-18

2 Wafalme 17:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika mwaka wa kumi na mbili wa enzi ya mfalme Ahazi wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka tisa. Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu ingawa siyo kama wafalme wa Israeli waliomtangulia. Mfalme Shalmanesa wa Ashuru alimshambulia; naye Hoshea akawa mtumishi wake na kumlipa ushuru. Lakini wakati mmoja Hoshea alituma wajumbe kwa mfalme wa Misri akiomba msaada; ndipo akaacha kulipa ushuru kwa mfalme Shalmanesa wa Ashuru kama alivyozoea kufanya kila mwaka. Shalmanesa alipoona hivi alimfunga Hoshea kwa minyororo na kumweka gerezani. Kisha mfalme wa Ashuru akaivamia nchi nzima na kuufikia mji wa Samaria na kuuzingira kwa muda wa miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea, mfalme wa Ashuru aliuteka Samaria, na kuwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru, baadhi yao akawaweka katika mji wa Hala, wengine karibu na mto Habori, mto Gozani na wengine katika miji ya Media. Haya yote yalitendeka kwa sababu watu wa Israeli walimwasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, ambaye aliwatoa kutoka mikononi mwa mfalme wa Misri, pia waliabudu miungu mingine, na kufuata njia za mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli, na kufanya matendo ya wafalme wa Israeli waliyoyaingiza nchini. Watu wa Israeli walitenda kwa siri mambo yasiyokuwa mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walijenga mahali pa juu pa kuabudia miungu ya uongo katika kila mji, kuanzia mnara wa walinzi mashambani hadi katika mji wenye ngome. Juu ya kila kilima na chini ya kila mti wenye majani mabichi, walijenga nguzo za mawe na sanamu za mungu wa kike Ashera, na wakafukiza ubani kwenye madhabahu zote za miungu ya uongo kufuatia desturi za mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yao maovu, na walitumikia sanamu ambazo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza, akisema, “Msifanye hivyo.” Mwenyezi-Mungu alituma manabii na waonaji kuionya Israeli na Yuda akisema, “Acheni njia zenu mbaya mkatii amri zangu na maagizo yangu kufuatana na sheria nilizowapa babu zenu, na ambazo niliwapeni kupitia kwa watumishi wangu manabii.” Lakini wao hawakutii; walikuwa wagumu kama babu zao ambao hawakumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walikataa kutii maagizo yake; hawakushika agano alilofanya na babu zao; licha ya kupuuza maonyo yake, waliabudu sanamu zisizokuwa na maana mpaka hata wao wenyewe hawakuwa na maana tena; walifuata desturi za mataifa yaliyowazunguka: Walipuuza amri za Mwenyezi-Mungu; wala hawakuzizingatia. Walivunja amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakatengeneza sanamu za miungu ya ndama wawili wa kusubu; vilevile wakatengeneza sanamu za mungu wa kike Ashera wakaabudu na vitu vyote vya angani na wakamtumikia Baali. Waliwatambika watoto wao wa kiume na wa kike kwa miungu ya uongo; wakataka shauri kwa watabiri na wachawi. Walinuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakamkasirisha sana. Basi, Mwenyezi-Mungu akawakasirikia sana watu wa Israeli na kuwafukuza kabisa mbele yake; hakuacha mtu isipokuwa kabila la Yuda peke yake.

2 Wafalme 17:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Katika mwaka wa kumi na mbili wa Ahazi mfalme wa Yuda Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka tisa. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, ila si kama wafalme wa Israeli waliomtangulia. Naye Shalmanesa mfalme wa Ashuru akakwea juu yake, Hoshea akawa mtumishi wake, akampa kodi. Mfalme wa Ashuru akaona fitina katika huyo Hoshea; kwa maana alikuwa ametuma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, wala hakumletea kodi mfalme wa Ashuru, kama alivyofanya mwaka kwa mwaka; kwa hiyo mfalme wa Ashuru akamfunga, akamtia kifungoni. Ndipo mfalme wa Ashuru akakwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya BWANA, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine. Wakaziendea sheria za mataifa, ambao BWANA aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya. Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya BWANA, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma. Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao BWANA aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe BWANA; wakatumikia sanamu, ambazo BWANA aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili. Pamoja na hayo BWANA aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu. Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini BWANA, Mungu wao. Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao BWANA alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao. Wakaziacha amri zote za BWANA, Mungu wao, wajitengenezea sanamu za kusubu, yaani, ndama wawili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali. Wakawapitisha watoto wao, wa kiume na wa kike, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza wenyewe wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha. Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila la Yuda peke yake.

2 Wafalme 17:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Katika mwaka wa kumi na mbili wa Ahazi mfalme wa Yuda Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kenda. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, ila si kama wafalme wa Israeli waliomtangulia. Naye Shalmanesa mfalme wa Ashuru akakwea juu yake, Hoshea akawa mtumishi wake, akampa kodi. Mfalme wa Ashuru akaona fitina katika huyo Hoshea; kwa maana alikuwa ametuma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, wala hakumletea kodi mfalme wa Ashuru, kama alivyofanya mwaka kwa mwaka; kwa hiyo mfalme wa Ashuru akamfunga, akamtia kifungoni. Ndipo mfalme wa Ashuru akakwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu. Katika mwaka wa kenda wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya BWANA, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine. Wakaziendea sheria za mataifa, ambao BWANA aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya. Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya BWANA, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma. Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao BWANA aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe BWANA; wakatumikia sanamu, ambazo BWANA aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili. Pamoja na hayo BWANA aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu. Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini BWANA, Mungu wao. Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao BWANA alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao. Wakaziacha amri zote za BWANA, Mungu wao, wakajifanyizia sanamu za kusubu, yaani, ndama mbili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali. Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha. Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake.

2 Wafalme 17:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Ahazi mfalme wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, akatawala kwa miaka tisa. Akafanya maovu machoni pa BWANA, lakini si kama wafalme wengine wa Israeli waliomtangulia. Mfalme Shalmanesa wa Ashuru akainuka dhidi ya Mfalme Hoshea, ambaye hapo mbeleni alikuwa mtumwa wake na kumlipa ushuru. Lakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri, naye hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumtia gerezani. Mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akapigana dhidi ya Samaria na kuizunguka kwa majeshi miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaiteka Samaria na kuwahamishia Waisraeli huko Ashuru. Akawaweka huko Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi. Yote haya yalitokea kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya BWANA Mungu wao, ambaye alikuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine na kufuata desturi za mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta. Waisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya BWANA Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye maboma walijijengea wenyewe mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote. Wakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda. Wakafukiza uvumba kila mahali palipoinuka, kama yalivyofanya yale mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha BWANA. Wakaabudu sanamu, ingawa BWANA alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.” BWANA akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Shikeni amri na maagizo yangu, kufuatana na sheria yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu manabii.” Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumtegemea BWANA Mungu wao. Walizikataa amri zake, na agano alilokuwa amelifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu zisizofaa, nao wenyewe wakawa hawafai. Wakayaiga mataifa yaliyowazunguka, ingawa BWANA alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya,” nao wakafanya mambo ambayo BWANA alikuwa amewakataza wasifanye. Wakayaacha maagizo yote ya BWANA Mungu wao na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali. Wakawatoa kafara wana wao na mabinti zao katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa BWANA, wakamghadhibisha. Basi BWANA akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki