2 Wafalme 17:1-18
2 Wafalme 17:1-18 BHN
Katika mwaka wa kumi na mbili wa enzi ya mfalme Ahazi wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka tisa. Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu ingawa siyo kama wafalme wa Israeli waliomtangulia. Mfalme Shalmanesa wa Ashuru alimshambulia; naye Hoshea akawa mtumishi wake na kumlipa ushuru. Lakini wakati mmoja Hoshea alituma wajumbe kwa mfalme wa Misri akiomba msaada; ndipo akaacha kulipa ushuru kwa mfalme Shalmanesa wa Ashuru kama alivyozoea kufanya kila mwaka. Shalmanesa alipoona hivi alimfunga Hoshea kwa minyororo na kumweka gerezani. Kisha mfalme wa Ashuru akaivamia nchi nzima na kuufikia mji wa Samaria na kuuzingira kwa muda wa miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea, mfalme wa Ashuru aliuteka Samaria, na kuwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru, baadhi yao akawaweka katika mji wa Hala, wengine karibu na mto Habori, mto Gozani na wengine katika miji ya Media. Haya yote yalitendeka kwa sababu watu wa Israeli walimwasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, ambaye aliwatoa kutoka mikononi mwa mfalme wa Misri, pia waliabudu miungu mingine, na kufuata njia za mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli, na kufanya matendo ya wafalme wa Israeli waliyoyaingiza nchini. Watu wa Israeli walitenda kwa siri mambo yasiyokuwa mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walijenga mahali pa juu pa kuabudia miungu ya uongo katika kila mji, kuanzia mnara wa walinzi mashambani hadi katika mji wenye ngome. Juu ya kila kilima na chini ya kila mti wenye majani mabichi, walijenga nguzo za mawe na sanamu za mungu wa kike Ashera, na wakafukiza ubani kwenye madhabahu zote za miungu ya uongo kufuatia desturi za mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yao maovu, na walitumikia sanamu ambazo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza, akisema, “Msifanye hivyo.” Mwenyezi-Mungu alituma manabii na waonaji kuionya Israeli na Yuda akisema, “Acheni njia zenu mbaya mkatii amri zangu na maagizo yangu kufuatana na sheria nilizowapa babu zenu, na ambazo niliwapeni kupitia kwa watumishi wangu manabii.” Lakini wao hawakutii; walikuwa wagumu kama babu zao ambao hawakumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walikataa kutii maagizo yake; hawakushika agano alilofanya na babu zao; licha ya kupuuza maonyo yake, waliabudu sanamu zisizokuwa na maana mpaka hata wao wenyewe hawakuwa na maana tena; walifuata desturi za mataifa yaliyowazunguka: Walipuuza amri za Mwenyezi-Mungu; wala hawakuzizingatia. Walivunja amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakatengeneza sanamu za miungu ya ndama wawili wa kusubu; vilevile wakatengeneza sanamu za mungu wa kike Ashera wakaabudu na vitu vyote vya angani na wakamtumikia Baali. Waliwatambika watoto wao wa kiume na wa kike kwa miungu ya uongo; wakataka shauri kwa watabiri na wachawi. Walinuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakamkasirisha sana. Basi, Mwenyezi-Mungu akawakasirikia sana watu wa Israeli na kuwafukuza kabisa mbele yake; hakuacha mtu isipokuwa kabila la Yuda peke yake.