Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 17

17
Hoshea, mfalme wa mwisho wa Israeli
1Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Ahazi mfalme wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miaka tisa. 2Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, lakini si kama wafalme wengine wa Israeli waliomtangulia.
3Mfalme Shalmanesa wa Ashuru akaenda na kumshambulia Mfalme Hoshea, ambaye hapo awali alikuwa akimlipa ushuru kwa sababu alikuwa mtumishi wake. 4Lakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri. Wala hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumfunga gerezani.
5Mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akapigana dhidi ya Samaria na kuuzingira kwa miaka mitatu.
Israeli kutekwa kwa sababu ya dhambi
6Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaiteka Samaria na kuwahamishia Waisraeli huko Ashuru. Akawakalisha huko Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi.
7Yote haya yalitukia kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, aliyekuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine, 8na kufuata desturi za mataifa ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta. 9Waisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye ngome, walijijengea mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote. 10Wakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda. 11Wakafukiza uvumba kila mahali pa juu pa kuabudia, kama yalivyofanya yale mataifa ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha Mwenyezi Mungu. 12Wakatumikia sanamu, ingawa Mwenyezi Mungu alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.” 13Mwenyezi Mungu akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Shikeni amri na maagizo yangu, kufuatana na Torati yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii, na ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu, manabii.”
14Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumwamini Mwenyezi Mungu, Mungu wao. 15Walizikataa amri zake, na agano alilolifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu batili, nao wenyewe wakawa batili. Wakayaiga mataifa yaliyowazunguka, ingawa Mwenyezi Mungu alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya.”
16Wakayaacha maagizo yote ya Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali. 17Wakawatoa kafara watoto wao wa kiume na wa kike katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa Mwenyezi Mungu, wakamghadhibisha.
18Basi Mwenyezi Mungu akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki. 19Hata hivyo, Yuda nao hawakuzishika amri za Mwenyezi Mungu, Mungu wao. Wakafuata desturi ambazo Israeli walikuwa wamezianzisha. 20Kwa hiyo Mwenyezi Mungu aliwakataa watu wote wa Israeli; akawatesa na kuwaachia katika mikono ya wateka nyara hadi alipowaondoa kwenye uwepo wake.
21Alipokwisha kuwatenga Israeli mbali na nyumba ya Daudi, wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme wao. Yeroboamu akawashawishi Israeli waache kumfuata Mwenyezi Mungu na akawasababisha kutenda dhambi kuu. 22Nao Israeli wakadumu katika dhambi zote za Yeroboamu mwana wa Nebati, nao hawakuziacha 23hadi Mwenyezi Mungu alipowaondoa kwenye uwepo wake, kama vile alivyokuwa ameonya kupitia watumishi wake wote manabii. Hivyo watu wa Israeli wakaondolewa kutoka nchi yao kwenda uhamishoni Ashuru, nao wako huko hata leo.
Samaria inakaliwa tena
24Mfalme wa Ashuru akawaleta watu kutoka Babeli, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria badala ya Waisraeli. Wakaimiliki Samaria na kuishi katika miji yake. 25Wakati walianza kuishi humo, hawakumwabudu Mwenyezi Mungu, kwa hiyo akatuma simba miongoni mwao, wakawaua baadhi ya watu. 26Habari ikapelekwa kwa mfalme wa Ashuru, kusema: “Watu uliowahamisha na kuwaweka katika miji ya Samaria hawajui kile Mungu wa nchi hiyo anachokitaka. Ametuma simba miongoni mwao, ambao wanawaua, kwa sababu watu hawajui anachokitaka.”
27Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru hivi: “Mtwae mmoja wa makuhani uliowachukua mateka kutoka Samaria ili arudi kuishi humo na awafundishe watu kile ambacho Mungu wa nchi anataka.” 28Basi mmoja wa makuhani aliyekuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Samaria akaja kuishi Betheli, akawafundisha jinsi ya kumwabudu Mwenyezi Mungu.
29Hata hivyo, kila kikundi cha taifa lililoletwa Samaria kilitengeneza miungu yao wenyewe katika miji kadhaa mahali walipoishi, nao wakaiweka katika nyumba za ibada za sanamu ambazo watu wa Samaria walikuwa wametengeneza katika mahali pa juu pa kuabudia. 30Watu kutoka Babeli wakatengeneza Sukoth-Benothi kuwa mungu wao, watu kutoka Kutha wakatengeneza Nergali, na watu kutoka Hamathi wakatengeneza Ashima; 31Waavi wakatengeneza Nibhazi na Tartaki, nao Wasefarvi wakachoma watoto wao kama kafara kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. 32Walimwabudu Mwenyezi Mungu, lakini pia waliteua aina zote za watu wao ili kuwawakilisha kama makuhani katika mahali pa ibada kwenye mahali pa juu pa kuabudia. 33Walimwabudu Mwenyezi Mungu, lakini pia waliitumikia miungu yao kulingana na desturi za mataifa walikotoka.
34Hadi leo wanashikilia desturi zao za zamani. Hawamwabudu Mwenyezi Mungu wala kuzishika hukumu na maagizo, sheria na amri ambazo Mwenyezi Mungu aliwapa uzao wa Yakobo, ambaye alimwita Israeli. 35Mwenyezi Mungu alipofanya agano na Waisraeli, aliwaamuru: “Msiiabudu miungu mingine yoyote wala kuisujudia, wala kuitumikia wala kuitolea dhabihu. 36Bali imewapasa kumwabudu Mwenyezi Mungu aliyewapandisha kutoka Misri kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake ulionyooshwa. Kwake yeye mtasujudu, na kwake yeye mtatoa dhabihu. 37Imewapasa daima kuwa waangalifu kutunza hukumu na maagizo, sheria na amri alizowaandikia. Msiabudu miungu mingine. 38Msisahau agano nililofanya nanyi, wala msiabudu miungu mingine. 39Bali, mtamwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwani yeye ndiye atakayewakomboa kutoka mikononi mwa adui zenu wote.”
40Hata hivyo hawakusikiliza, lakini waliendelea na desturi zao za awali. 41Hata wakati watu hawa walipokuwa wanamwabudu Mwenyezi Mungu, walikuwa bado wakitumikia sanamu zao. Hadi leo watoto wao na wajukuu wao wanaendelea kufanya kama baba zao walivyofanya.

Iliyochaguliwa sasa

2 Wafalme 17: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia