2 Wafalme 18
18
Hezekia mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 29:1–31:21)
1Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Hoshea mwana wa Ela mfalme wa Israeli, Hezekia mwana wa Ahazi mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Abiya binti Zekaria. 3Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, kama Daudi baba yake alivyofanya. 4Akapaondoa mahali pa juu pa kuabudia, akazivunja sanamu, akakatakata nguzo za Ashera. Akavunja vipande vipande ile nyoka ya shaba Musa aliyotengeneza, kwa kuwa hadi siku hizo Waisraeli walikuwa wanaifukizia uvumba. (Ilikuwa ikiitwa Nehushtani#18:4 maana yake Kipande cha shaba).
5Hezekia aliweka tumaini lake kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Hapakuwa na mfalme mwingine wa kufanana naye miongoni mwa wafalme wa Yuda, kabla yake au baada yake. 6Alishikamana na Mwenyezi Mungu kwa bidii wala hakuacha kumfuata; alishika amri ambazo Mwenyezi Mungu alikuwa amempa Musa. 7Naye Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja naye, akafanikiwa katika kila alichokifanya. Aliasi dhidi ya mfalme wa Ashuru, wala hakumtumikia. 8Kuanzia mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye ngome, aliwashinda Wafilisti, hadi kufikia Gaza na himaya yake yote.
9Mwaka wa nne wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa saba wa Hoshea mwana wa Ela kutawala Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru alienda kushambulia Samaria na kuuzingira. 10Baada ya miaka mitatu Waashuru wakautwaa. Kwa hiyo Samaria ulitekwa katika mwaka wa sita wa utawala wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea mfalme wa Israeli. 11Mfalme wa Ashuru akawahamishia Waisraeli huko Ashuru na akawaweka Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi. 12Hili lilitokea kwa sababu hawakumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wao, lakini walikuwa wamevunja agano lake, yale yote ambayo Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliwaamuru. Hawakuzisikiliza amri wala kuzitimiza.
13Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka. 14Basi Hezekia mfalme wa Yuda akamtumia ujumbe mfalme wa Ashuru huko Lakishi akisema: “Nimefanya makosa. Ondoka katika nchi yangu, nami nitakulipa chochote unachokitaka kwangu.” Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia mfalme wa Yuda talanta mia tatu#18:14 Talanta 300 ni sawa na tani 10. za fedha, na talanta thelathini#18:14 Talanta 30 ni sawa na tani moja. za dhahabu. 15Basi Hezekia akampa fedha yote iliyopatikana ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na katika hazina ya jumba la mfalme.
16Wakati huu Hezekia mfalme wa Yuda akabandua dhahabu yote iliyokuwa imefunika milango na miimo ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, akampa mfalme wa Ashuru.
Senakeribu anaitishia Yerusalemu
(2 Nyakati 32:1-19; Isaya 36:1-22)
17Mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wake mkuu, na afisa wake mkuu, na jemadari wa jeshi, pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Wakaja Yerusalemu na kusimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi. 18Wakaagiza mfalme aitwe. Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la mfalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakawaendea.
19Yule jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia:
“ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako? 20Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi? 21Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea. 22Nawe ukiniambia, “Tunamtumainia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu”: je, siyo yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya katika Yerusalemu”?
23“ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao! 24Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi? 25Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza mahali hapa pasipo neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”
26Ndipo Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania, watu walio juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”
27Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mkojo wao wenyewe?”
28Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! 29Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa mkononi mwangu. 30Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini Mwenyezi Mungu kwa kuwaambia, ‘Hakika Mwenyezi Mungu atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’
31“Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe, 32hadi nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu, nchi ya mizeituni na asali. Chagueni uzima, sio mauti!
“Msimsikilize Hezekia, kwa kuwa anawapotosha asemapo, ‘Mwenyezi Mungu atatuokoa.’ 33Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru? 34Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu? 35Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Mwenyezi Mungu aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?”
36Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.”
37Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia vile jemadari wa jeshi alivyosema.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wafalme 18: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.