Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 7:1-10

2 Nyakati 7:1-10 NEN

Baada ya Solomoni kumaliza kuomba, moto ukashuka kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu, nao utukufu wa BWANA ukalijaza Hekalu. Makuhani hawakuweza kuingia ndani ya Hekalu la BWANA kwa sababu utukufu wa BWANA ulilijaza. Waisraeli wote walipoona moto ukishuka na utukufu wa BWANA ukiwa juu ya Hekalu, wakapiga magoti sakafuni wakasujudu nyuso zao mpaka chini, nao wakamwabudu na kumshukuru BWANA wakisema, “Yeye ni mwema; upendo wake unadumu milele.” Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za BWANA Mungu. Naye Mfalme Solomoni akatoa dhabihu ya ngʼombe 22,000 pamoja na kondoo na mbuzi 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na watu wote walivyoweka wakfu Hekalu la Mungu. Makuhani wakasimama kwenye nafasi zao, vivyo hivyo Walawi wakiwa na vyombo vya uimbaji vya BWANA ambavyo Mfalme Daudi alikuwa ametengeneza kwa ajili ya kumsifu BWANA, navyo vilitumika wakati aliposhukuru, akisema, “Upendo wake wadumu milele.” Mkabala na Walawi, makuhani walipiga tarumbeta zao, nao Waisraeli wote walikuwa wamesimama. Solomoni akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la BWANA na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba aliyokuwa ametengeneza haikutosha kuweka sadaka hizo zote za kuteketezwa, sadaka za nafaka na za mafuta. Hivyo Solomoni akaiadhimisha sikukuu wakati ule kwa muda wa siku saba, na Israeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Katika siku ya nane walifanya kusanyiko, kwa kuwa walikuwa wanaadhimisha kuwekwa wakfu kwa madhabahu kwa muda wa siku saba na sikukuu kwa muda wa siku nyingine saba zaidi. Katika siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa saba Solomoni akawaaga watu waende nyumbani mwao, wakishangilia na kufurahi mioyoni mwao, kwa wema mwingi BWANA Mungu aliomtendea Daudi na Solomoni na kwa ajili ya watu wake Israeli.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha