Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 7:1-10

2 Mambo ya Nyakati 7:1-10 SRUV

Basi Sulemani alipomaliza maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa BWANA ukaijaza nyumba. Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa BWANA, kwa kuwa utukufu wa BWANA umeijaza nyumba ya BWANA. Wana wa Israeli wote walipoona ule moto ukishuka, utukufu wa BWANA ulipokuwa katika nyumba, wakasujudu kifudifudi mpaka sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru BWANA, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele. Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za BWANA. Mfalme Sulemani akatoa sadaka ya ng'ombe elfu ishirini na mbili, na kondoo elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Mungu. Makuhani wakasimama kwenye nafasi zao walipoagizwa; Walawi nao pamoja na vinanda vya BWANA, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru BWANA, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama. Tena Sulemani akaitakasa behewa katikati, iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba aliyoifanya Sulemani haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta. Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba. Siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana waliadhimisha kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba. Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake.