Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 7:1-10

2 Mambo ya Nyakati 7:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Solomoni alipomaliza sala yake, moto ulishuka kutoka mbinguni na kuchoma sadaka na tambiko za kuteketeza zilizotolewa, kisha utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukaijaza nyumba. Kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulijaa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, makuhani hawakuweza kuingia humo. Waisraeli wote walipoona moto ukishuka kutoka mbinguni na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulijaa katika nyumba walisujudu nyuso zao zikifika mpaka sakafuni, wakamwabudu na kumshukuru Mwenyezi-Mungu wakisema, “Kwa kuwa ni mwema, fadhili zake zadumu milele.” Kisha mfalme Solomoni na watu wote walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko. Naye Solomoni alimtolea Bwana ng'ombe 22,000 na kondoo 120,000. Hivyo ndivyo Solomoni na watu wote walivyoiweka wakfu nyumba ya Mungu. Makuhani walisimama mahali maalumu walipoagizwa kusimama, nao Walawi walisimama wakiwa na vyombo vya Mwenyezi-Mungu vya muziki mfalme Daudi alivyovitengeneza kwa ajili ya kutoa shukrani kwa Mwenyezi-Mungu. Waliimba, “Kwa kuwa fadhili zake zadumu milele,” Daudi alivyowaagiza. Makuhani walipiga tarumbeta hali Waisraeli wote walikuwa wamesimama. Basi, mfalme Solomoni akaiweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kwani hapo ndipo alipotolea sadaka za kuteketezwa na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu ile madhabahu ya shaba haikutosha kwa sadaka hizo zote. Naye Solomoni kwa muda wa siku saba alifanya sikukuu pamoja na kusanyiko kubwa la watu wote wa Israeli waliotoka kiingilio cha Hamathi mpaka mto wa Misri. Siku ya nane, walikusanyika wakafanya ibada maalumu baada ya muda wa siku saba walizotumia kuitakasa meza ya matoleo ya sadaka, na siku saba nyingine za sikukuu. Siku iliyofuata ambayo ilikuwa siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa saba, Solomoni aliwaaga watu waende kwao, wakishangilia na kufurahi moyoni kwa sababu ya wema ambao Mwenyezi-Mungu aliowajalia Daudi, Solomoni na watu wake Israeli.

2 Mambo ya Nyakati 7:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Sulemani alipomaliza maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa BWANA ukaijaza nyumba. Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa BWANA, kwa kuwa utukufu wa BWANA umeijaza nyumba ya BWANA. Wana wa Israeli wote walipoona ule moto ukishuka, utukufu wa BWANA ulipokuwa katika nyumba, wakasujudu kifudifudi mpaka sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru BWANA, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele. Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za BWANA. Mfalme Sulemani akatoa sadaka ya ng'ombe elfu ishirini na mbili, na kondoo elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Mungu. Makuhani wakasimama kwenye nafasi zao walipoagizwa; Walawi nao pamoja na vinanda vya BWANA, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru BWANA, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama. Tena Sulemani akaitakasa behewa katikati, iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba aliyoifanya Sulemani haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta. Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba. Siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana waliadhimisha kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba. Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake.

2 Mambo ya Nyakati 7:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa BWANA ukaijaza nyumba. Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa BWANA, kwa kuwa utukufu wa BWANA umeijaza nyumba ya BWANA. Wakatazama wana wa Israeli wote, uliposhuka ule moto, utukufu wa BWANA ulipokuwapo juu ya nyumba; wakasujudu kifulifuli hata nchi sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru BWANA, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele. Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za BWANA. Mfalme Sulemani akatoa sadaka ya ng’ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Mungu. Wakasimama makuhani sawasawa na malinzi yao; Walawi nao pamoja na vinanda vya BWANA, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru BWANA, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama. Tena Sulemani akaitakasa behewa katikati, iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba aliyoifanya Sulemani haikutosha kuzipokea sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta. Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba. Hata siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana walishika kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba. Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake.

2 Mambo ya Nyakati 7:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya Solomoni kumaliza kuomba, moto ukashuka kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu, nao utukufu wa BWANA ukalijaza Hekalu. Makuhani hawakuweza kuingia ndani ya Hekalu la BWANA kwa sababu utukufu wa BWANA ulilijaza. Waisraeli wote walipoona moto ukishuka na utukufu wa BWANA ukiwa juu ya Hekalu, wakapiga magoti sakafuni wakasujudu nyuso zao mpaka chini, nao wakamwabudu na kumshukuru BWANA wakisema, “Yeye ni mwema; upendo wake unadumu milele.” Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za BWANA Mungu. Naye Mfalme Solomoni akatoa dhabihu ya ngʼombe 22,000 pamoja na kondoo na mbuzi 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na watu wote walivyoweka wakfu Hekalu la Mungu. Makuhani wakasimama kwenye nafasi zao, vivyo hivyo Walawi wakiwa na vyombo vya uimbaji vya BWANA ambavyo Mfalme Daudi alikuwa ametengeneza kwa ajili ya kumsifu BWANA, navyo vilitumika wakati aliposhukuru, akisema, “Upendo wake wadumu milele.” Mkabala na Walawi, makuhani walipiga tarumbeta zao, nao Waisraeli wote walikuwa wamesimama. Solomoni akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la BWANA na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba aliyokuwa ametengeneza haikutosha kuweka sadaka hizo zote za kuteketezwa, sadaka za nafaka na za mafuta. Hivyo Solomoni akaiadhimisha sikukuu wakati ule kwa muda wa siku saba, na Israeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Katika siku ya nane walifanya kusanyiko, kwa kuwa walikuwa wanaadhimisha kuwekwa wakfu kwa madhabahu kwa muda wa siku saba na sikukuu kwa muda wa siku nyingine saba zaidi. Katika siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa saba Solomoni akawaaga watu waende nyumbani mwao, wakishangilia na kufurahi mioyoni mwao, kwa wema mwingi BWANA Mungu aliomtendea Daudi na Solomoni na kwa ajili ya watu wake Israeli.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha