Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 36

36
Yehoahazi mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 23:30-35)
1Watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia na kumfanya mfalme mahali pa baba yake huko Yerusalemu.
2Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na tatu alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa miezi mitatu. 3Mfalme wa Misri akamwondoa madarakani huko Yerusalemu, na akatoza Yuda kodi ya talanta mia moja#36:3 Talanta 100 za fedha ni sawa na tani 3.75. za fedha, na talanta moja#36:3 Talanta moja ya dhahabu ni sawa na kilo 34. ya dhahabu. 4Mfalme wa Misri akamweka Eliakimu, nduguye Yehoahazi, kuwa mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu na kubadili jina la Eliakimu kuwa Yehoyakimu. Lakini Neko akamchukua Yehoahazi, nduguye Eliakimu, akampeleka Misri.
Yehoyakimu mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 23:35–24:7)
5Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wake. 6Nebukadneza mfalme wa Babeli akamshambulia na kumfunga kwa pingu za shaba akampeleka Babeli. 7Nebukadneza akachukua pia vyombo kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu na kuviweka katika hekalu lake#36:7 au: katika jumba lake la kifalme. huko Babeli.
8Matukio mengine ya utawala wa Yehoyakimu, machukizo aliyoyafanya na yote yaliyoonekana dhidi yake, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda. Naye Yehoyakini mwanawe akawa mfalme baada yake.
Yehoyakini mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 24:8-17)
9Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu na siku kumi. Akafanya yaliyo maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. 10Majira ya vuli, Mfalme Nebukadneza akatuma watu, nao wakamleta Babeli, pamoja na vyombo vya thamani kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu. Naye akamfanya Sedekia, ndugu yake Yehoyakimu kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu.
Sedekia mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 24:18-20; Yeremia 52:1-3)
11Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na moja. 12Alifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, wala hakujinyenyekeza mbele ya nabii Yeremia, ambaye alinena neno la Mwenyezi Mungu. 13Pia alimwasi Mfalme Nebukadneza, aliyekuwa amemwapisha kwa jina la Mungu. Akashupaza shingo na akafanya moyo wake kuwa mgumu wala hakutaka kumgeukia Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 14Zaidi ya hayo viongozi wote wa makuhani pamoja na watu wakazidi kukosa uaminifu zaidi na zaidi, wakafanya machukizo yote kama walivyofanya mataifa wakinajisi Hekalu la Mwenyezi Mungu alilokuwa amelitakasa huko Yerusalemu.
Kuanguka kwa Yerusalemu
(2 Wafalme 25:1-21; Yeremia 52:3-11)
15Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, akawapelekea neno kupitia wajumbe wake tena na tena, kwa sababu alikuwa anawahurumia watu wake pamoja na mahali pa Maskani yake. 16Lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mwenyezi Mungu wakayadharau maneno yake na kuwacheka manabii wake hadi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ikawa kubwa dhidi ya watu wake, na hakukuwa na namna ya kuituliza. 17Mungu akamwinua dhidi yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao wa kiume kwa upanga ndani ya mahali patakatifu. Hakumbakiza kijana wala mwanamwali, mzee wala mnyonge. Mungu akawatia wote mikononi mwa Nebukadneza. 18Akavichukua kwenda Babeli vyombo vyote kutoka Hekalu la Mungu, vikubwa na vidogo, hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu pamoja na hazina za mfalme na za maafisa wake. 19Wakalichoma Hekalu la Mungu na kuzibomoa kuta za Yerusalemu, wakachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu kila kitu chake cha thamani.
20Wale watu walionusurika kuuawa kwa upanga wakachukuliwa kwenda uhamishoni Babeli. Nao wakawa watumishi wake na wa wanawe hadi wakati wa utawala wa ufalme wa Uajemi ulifika. 21Nchi ikaendelea kufurahia pumziko zake za sabato; wakati wote wa kufanywa kwake ukiwa ilipumzika, hadi ile miaka sabini ilipotimia katika kutimiza neno la Mwenyezi Mungu lililonenwa na Yeremia.
Koreshi aruhusu watu kurudi Yerusalemu
(Ezra 1:1-4)
22Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, ili kulitimiza neno la Mwenyezi Mungu lililosemwa na nabii Yeremia, Mwenyezi Mungu aliusukuma moyo wa Koreshi mfalme wa Uajemi kutangaza katika himaya yake yote kwa maandishi:
23“Hili ndilo asemalo Koreshi mfalme wa Uajemi:
“ ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote duniani, na ameniagiza kumjengea Hekalu huko Yerusalemu katika Yuda. Yeyote kati ya watu wa Mungu miongoni mwenu, Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na awe pamoja naye, wacha apande.’ ”

Iliyochaguliwa sasa

2 Nyakati 36: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia