Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 35

35
Yosia aadhimisha Pasaka
(2 Wafalme 23:21-23)
1Yosia akaadhimisha Pasaka kwa Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu, mwana-kondoo wa Pasaka akachinjwa siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. 2Akawaweka makuhani kwenye wajibu wao na kuwatia moyo katika utumishi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu. 3Akawaambia Walawi, waliowafundisha Waisraeli wote na waliokuwa wamejiweka wakfu kwa ajili ya kazi ya Mwenyezi Mungu, “Liwekeni hilo Sanduku takatifu katika Hekalu lile alilojenga Sulemani mwana wa Daudi mfalme wa Israeli. Halipaswi kubebwa mabegani mwenu. Sasa mtumikieni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na watu wake Israeli. 4Jiandaeni kwa kufuata jamaa zenu katika migawanyo yenu, kufuatana na maelezo yaliyoandikwa na Daudi mfalme wa Israeli na mwanawe Sulemani.
5“Simameni mahali patakatifu kwa kufuata migawanyo ya jamaa za baba zenu kulingana na koo zenu na pawepo Walawi kwa ajili ya kila mgawanyo wa nyumba ya baba zenu. 6Chinjeni mwana-kondoo wa Pasaka, jitakaseni, nanyi kwa niaba ya koo zenu fanyeni maandalizi, mkitenda sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu kwa mkono wa Musa.”
7Ndipo Yosia akawapa watu wote waliokuwepo wana-mbuzi na kondoo wapatao elfu thelathini kwa ajili ya sadaka ya Pasaka, pia na ng’ombe elfu kumi; wote kutoka kwa mali binafsi ya mfalme.
8Pia maafisa wake, wakatoa kwa hiari yao wakawapa watu, makuhani na Walawi. Hilkia, Zekaria na Yehieli, waliokuwa maafisa wakuu wa Hekalu la Mungu, wakawapa makuhani sadaka za Pasaka wana-kondoo na wana-mbuzi elfu mbili na mia sita, na mafahali mia tatu. 9Konania na nduguze wawili, Shemaya na Nethaneli, pamoja na Hashabia, Yeieli na Yozabadi waliokuwa viongozi wa Walawi, nao pia wakawapa Walawi wana-kondoo na wana-mbuzi elfu tano, na mafahali mia tano, kwa ajili ya sadaka za Pasaka.
10Huduma ilipomalizika kuandaliwa makuhani wakasimama mahali pao na Walawi katika migawanyo yao kama mfalme alivyokuwa ameamuru. 11Wana-kondoo wa Pasaka wakachinjwa, nao makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa, wakati Walawi wakiwa wanawachuna wale wanyama ngozi. 12Wakatenga sadaka za kuteketezwa ili waweze kugawia ili migawanyo kwa kufuata jamaa za baba zao ili watoe sadaka kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Musa. Wakafanya vivyo hivyo kwa wale mafahali. 13Wakawaoka wale wanyama wa Pasaka kwenye moto kama ilivyoamriwa, wakachemsha zile sadaka takatifu kwenye vyungu, masufuria makubwa na vikaango na kuwagawia watu wote upesi. 14Hatimaye wakafanya maandalizi kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani, kwa sababu wale makuhani, yaani wazao wa Haruni, walikuwa wanatoa sadaka za kuteketezwa pamoja na zile sehemu zilizonona hadi usiku. Hivyo Walawi wakafanya maandalizi kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani wa uzao wa Haruni.
15Waimbaji, wazao wa Asafu, walikuwa katika nafasi zao, kama ilivyoagizwa na Mfalme Daudi, Asafu, Hemani na Yeduthuni mwonaji wa Mfalme. Mabawabu katika kila lango hawakuhitaji kuacha nafasi zao kwa sababu Walawi wenzao walifanya maandalizi kwa ajili yao.
16Kwa hiyo wakati ule, huduma yote ya Mwenyezi Mungu ilifanyika katika kuadhimisha Pasaka, na kutoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, kama alivyoamuru Mfalme Yosia. 17Waisraeli waliokuwepo wakaadhimisha Pasaka wakati huo na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa siku saba. 18Kulikuwa hakujafanyika Pasaka kama hii katika Israeli tangu siku za nabii Samweli wala hakukuwa na mfalme yeyote wa Israeli ambaye kamwe alishaadhimisha Pasaka kama ile aliyofanya Mfalme Yosia, akiwa na makuhani, Walawi, na watu wote wa Yuda na wa Israeli waliokuwa huko, pamoja na wakaaji wa Yerusalemu. 19Pasaka iliadhimishwa katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia.
Kifo cha Yosia
(2 Wafalme 23:28-30)
20Baada ya haya yote, Yosia alipomaliza kulitengeneza vizuri Hekalu, Neko mfalme wa Misri akapanda ili kupigana huko Karkemishi katika Mto Frati, naye Yosia akatoka kwenda kupigana naye. 21Lakini Neko akamtumia wajumbe kusema, “Kuna ugomvi gani kati yangu mimi na wewe, ee mfalme wa Yuda? Si wewe ninayekushambulia wakati huu, bali ile nyumba niliyo na vita nayo, Mungu ameniambia niharakishe, kwa hivyo acha kumpinga Mungu, ambaye yuko pamoja nami, la sivyo atakuangamiza.”
22Lakini hata hivyo, Yosia hakukubali kumwacha, bali alijibadilisha ili kupigana naye vita. Hakusikiliza yale Neko aliyokuwa amemwambia kwa agizo la Mungu bali alienda kupigana naye katika tambarare ya Megido.
23Wapiga upinde wakampiga Mfalme Yosia, naye akawaambia maafisa wake, “Niondoeni, nimejeruhiwa vibaya sana.” 24Kwa hiyo wakamshusha kutoka gari lake la vita, wakamweka kwenye gari lingine alilokuwa nalo na kumleta Yerusalemu, ambako alifia. Akazikwa katika makaburi ya baba zake, nayo Yuda yote na Yerusalemu wakamwombolezea Yosia.
25Nabii Yeremia akatunga maombolezo kwa ajili ya kifo chake, nao waimbaji wote, wanaume kwa wanawake, hufanya ukumbusho wa Yosia katika maombolezo hadi leo. Haya yakafanywa desturi katika Israeli, nayo yameandikwa katika Maombolezo.
26Matukio mengine ya utawala wa Yosia na matendo yake mema, kulingana na yale yaliyoandikwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu: 27matukio yote, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.

Iliyochaguliwa sasa

2 Nyakati 35: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia