Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 33

33
Manase mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 21:1-18)
1Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na tano. 2Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli. 3Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia ambapo Hezekia baba yake, alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Mabaali na nguzo za Maashera. Akayasujudia majeshi yote ya angani na kuyaabudu. 4Akajenga madhabahu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu ambamo Mwenyezi Mungu alikuwa amesema, “Jina langu litadumu Yerusalemu milele.” 5Katika nyua zote mbili za Hekalu la Mwenyezi Mungu akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani. 6Akawatoa kafara watoto wake kwa kuwapitishia motoni katika Bonde la Ben-Hinomu; akafanya ulozi, uaguzi, na uchawi, akatafuta ushauri kwa wenye pepo wa utambuzi na wenye kuwasiliana na mizimu. Akafanya maovu mengi machoni pa Mwenyezi Mungu, akaichochea hasira yake.
7Akachukua ile sanamu aliyoichonga na kuiweka katika Hekalu la Mungu ambalo Mungu alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Sulemani, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu, mji niliouchagua kutoka makabila yote ya Israeli, nitaliweka Jina langu milele. 8Sitaifanya tena miguu ya Waisraeli iondoke tena katika nchi niliyowapa baba zenu, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru kuhusu sheria zote, maagizo na amri zilizotolewa kwa mkono wa Musa.” 9Lakini Manase akawaongoza Yuda na watu wa Yerusalemu katika upotovu, kiasi kwamba walifanya maovu mengi kuliko mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliangamiza mbele ya Waisraeli.
10Mwenyezi Mungu akasema na Manase pamoja na watu wake, lakini hawakumjali. 11Hivyo Mwenyezi Mungu akaleta juu yao majemadari wa jeshi la mfalme wa Ashuru, ambao walimchukua Manase kwenda kifungoni, wakaweka ndoana katika pua yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli. 12Katika dhiki yake akamsihi Mwenyezi Mungu, Mungu wake, na kujinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake. 13Naye alipomwomba, Mwenyezi Mungu akaguswa na kule kusihi kwake na akasikiliza dua lake. Kwa hiyo akamrudisha Yerusalemu na kwenye ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mungu.
14Baadaye akajenga ukuta wa nje wa Mji wa Daudi, magharibi mwa chemchemi ya Gihoni katika bonde, hadi kufikia ingilio la Lango la Samaki na akakizunguka kilima cha Ofeli; pia akaufanya mrefu zaidi. Akawaweka majemadari katika miji yote ya Yuda iliyokuwa imejengewa ngome.
15Akaondolea mbali miungu ya kigeni pamoja na sanamu kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu. Pia akaondoa madhabahu zote alizojenga katika kilima kilichojengwa Hekalu, na katika Yerusalemu, akazitupa nje ya mji. 16Kisha akarudisha madhabahu ya Mwenyezi Mungu na kutolea juu yake dhabihu za sadaka za amani pamoja na sadaka za shukrani, naye akawaamuru Yuda wamtumikie Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 17Hata hivyo watu wakaendelea kutoa dhabihu mahali pa juu pa kuabudia, lakini wakawa wakimtolea Mwenyezi Mungu, Mungu wao, peke yake.
18Matukio mengine ya utawala wa Manase, maombi yake kwa Mungu wake na maneno aliyoambiwa na waonaji walionena naye kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. 19Maombi yake, pamoja na jinsi Mungu alivyoguswa na kusihi kwake, pia dhambi zake zote na kukosa uaminifu kwake, pamoja na sehemu alizojenga mahali pa juu pa kuabudia, na kusimamisha nguzo za Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekeza kwake: haya yote yameandikwa katika kumbukumbu za waonaji. 20Manase akalala na baba zake, akazikwa katika jumba lake la kifalme. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
Amoni mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 21:19-26)
21Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. 22Akatenda maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba yake Manase alivyofanya. Amoni akaabudu na kutoa dhabihu kwa sanamu zote alizokuwa ametengeneza Manase. 23Lakini tofauti na Manase baba yake, hakujinyenyekeza mbele za Mwenyezi Mungu, badala yake Amoni alijiongeza hatia zaidi.
24Watumishi wa Amoni wakampangia njama, nao wakamuua ndani ya jumba lake la kifalme. 25Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamepanga njama dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake.

Iliyochaguliwa sasa

2 Nyakati 33: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia