Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 32

32
Senakeribu atishia Yerusalemu
(2 Wafalme 18:13-37; 19:14-19, 35-37; Isaya 36:1-22; 37:8-38)
1Baada ya yale yote aliyokuwa amefanya Hezekia kwa uaminifu mkubwa, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaja na kuvamia Yuda. Akaizingira miji yenye ngome, akikusudia kuiteka iwe yake. 2Hezekia alipoona kuwa Senakeribu amekuja na kwamba alikusudia kufanya vita juu ya Yerusalemu, 3akafanya shauri na maafisa wake na mashujaa wake juu ya kuzuia maji kutoka chemchemi zilizo nje ya mji, nao wakamsaidia. 4Umati mkubwa wa watu wakakusanyika na kuzuia chemchemi zote na vijito vilivyotiririka katika nchi yote, wakisema: “Kwa nini wafalme wa Ashuru waje na kukuta maji tele?” 5Hezekia akafanya kazi kwa bidii kukarabati sehemu zote zilizokuwa zimebomoka za ukuta na kujenga minara juu yake. Akajenga ukuta mwingine nje ya ule uliokuwako, na kuimarisha Milo#32:5 Milo maana yake Boma la Ngome. katika Mji wa Daudi. Akatengeneza pia silaha nyingi na ngao.
6Akaweka maafisa wa jeshi juu ya watu, wakawakutanisha mbele yake katika uwanja kwenye lango la mji, naye akawatia moyo kwa maneno haya: 7“Kuweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye. 8Kwake uko mkono wa mwili tu, bali kwetu yuko Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Nao watu wakatiwa moyo kutokana na maneno aliyowaambia Hezekia mfalme wa Yuda.
9Hatimaye Senakeribu mfalme wa Ashuru na majeshi yake yote walipokuwa wameuzingira Lakishi, akawatuma maafisa wake kwenda Yerusalemu wakiwa na ujumbe huu kwa Hezekia mfalme wa Yuda, na kwa watu wote wa Yuda waliokuwa humo, kusema:
10“Hili ndilo asemalo Senakeribu mfalme wa Ashuru: Je, mmeweka tumaini lenu wapi, hata mnaendelea kukaa katika Yerusalemu, hali mmezingirwa na jeshi? 11Hezekia asemapo, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, atatuokoa kutoka mkononi wa mfalme wa Ashuru,’ anawapotosha ninyi, naye atawaacha mfe kwa njaa na kiu. 12Je, si Hezekia mwenyewe aliyeondoa mahali pa juu pa kuabudia pamoja na madhabahu zake, akiwaambia Yuda wa Yerusalemu, ‘Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu moja na kuteketeza dhabihu juu yake’?
13“Je, hamjui yale mimi na baba zangu tuliyoyafanya kwa mataifa yote ya nchi zingine? Je, miungu ya mataifa hayo iliweza kuokoa nchi zao kutoka mkononi mwangu? 14Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya mataifa haya ambayo baba zangu waliyaangamiza ameweza kuwaokoa watu wake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Mungu wenu kuwaokoa mkononi mwangu? 15Sasa basi, msikubali Hezekia awadanganye na kuwapotosha namna hii. Msimwamini, kwa kuwa hakuna mungu wa taifa lolote wala wa ufalme wowote aliyeweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu au mkononi mwa baba zangu. Sembuse huyo mungu wenu atawaokoaje kutoka mkononi mwangu!”
16Maafisa wa Senakeribu wakaendelea kunena dhidi ya Bwana Mwenyezi Mungu na dhidi ya mtumishi wake Hezekia. 17Mfalme pia aliandika barua akimtukana Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, na kusema haya dhidi yake: “Kama vile miungu ya mataifa ya nchi nyingine ilivyoshindwa kuwaokoa watu wao mkononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu.” 18Kisha wakawaita kwa Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa juu ya ukuta ili kuwatisha na kuwatia hofu ili waweze kuuteka mji. 19Wakanena kuhusu Mungu wa Yerusalemu kama vile walivyonena kuhusu miungu ya mataifa mengine ya dunia ambayo ni kazi ya mikono ya wanadamu.
20Mfalme Hezekia na nabii Isaya mwana wa Amozi wakalilia mbingu katika maombi kuhusu jambo hili. 21Naye Mwenyezi Mungu akamtuma malaika ambaye aliangamiza wapiganaji wote, na viongozi na maafisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Kwa hiyo, mfalme wa Ashuru akarudi nchini mwake kwa aibu. Naye alipoenda katika hekalu la mungu wake, baadhi ya watoto wake mwenyewe wakamuua kwa upanga.
22Hivyo Mwenyezi Mungu akamwokoa Hezekia na watu wa Yerusalemu kutoka mkononi mwa Senakeribu mfalme wa Ashuru na kutoka mikononi mwa wengine wote. Mwenyezi Mungu akawapa amani pande zote. 23Watu wengi wakaleta sadaka Yerusalemu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na zawadi za thamani kwa ajili ya Hezekia mfalme wa Yuda. Tangu hapo na kuendelea, Hezekia aliheshimiwa sana na mataifa yote.
Kiburi cha Hezekia, mafanikio na kifo
(2 Wafalme 20:1-3, 12-19; Isaya 38:1-3; 39:1-8)
24Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Akamwomba Mwenyezi Mungu, ambaye alimjibu na kumpa ishara. 25Lakini moyo wa Hezekia ukajaa majivuno na hakuonesha itikio kwa wema aliotendewa, kwa hiyo ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ikawa juu yake na juu ya Yuda na Yerusalemu. 26Ndipo Hezekia akatubu kwa ajili ya kiburi cha moyo wake, kama walivyofanya watu wa Yerusalemu, kwa hiyo ghadhabu ya Mwenyezi Mungu haikuja juu yao katika siku za Hezekia.
27Hezekia alikuwa na utajiri mwingi sana na heshima, naye akajifanyia hazina kwa ajili ya fedha yake na dhahabu na kwa ajili ya vito vyake vya thamani, vikolezo, ngao na aina zote za vyombo vya thamani. 28Akajenga pia maghala ya kuhifadhi mavuno ya nafaka, divai mpya na mafuta. Akatengeneza mabanda kwa ajili ya aina mbalimbali za mifugo, na mazizi kwa ajili ya kondoo na mbuzi. 29Akajenga vijiji na kujipatia idadi kubwa ya kondoo na mbuzi, pamoja na ng’ombe, kwa kuwa Mungu alikuwa amempa utajiri mwingi sana.
30Hezekia ndiye aliziba njia za kutolea maji za chemchemi za juu za Gihoni na kuyaelekeza maji kutiririkia upande wa magharibi wa Mji wa Daudi. Akafanikiwa katika kila kitu alichofanya. 31Lakini wajumbe walipotumwa na watawala wa Babeli kumuuliza kuhusu ishara ambayo ilifanyika nchini, Mungu alimwacha ili kumjaribu na kujua kila kitu kilichokuwa moyoni mwake.
32Matukio mengine ya utawala wa Hezekia na matendo yake ya kujitoa kwa moyo yameandikwa katika maono ya nabii Isaya mwana wa Amozi kwenye kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli. 33Hezekia akalala na baba zake na akazikwa kwenye kilima mahali yalipo makaburi ya wazao wa Daudi. Yuda wote na watu wa Yerusalemu wakamheshimu alipofariki. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.

Iliyochaguliwa sasa

2 Nyakati 32: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia