1 Wathesalonike Utangulizi
Utangulizi
Paulo katika safari yake ya pili kueneza Injili alitembelea mji wa Thesalonike, ambao ulikuwa kituo cha biashara. Alihudumu huko kwa majuma matatu, akahubiri katika sinagogi la Wayahudi, akithibitisha kutoka Maandiko ya Agano la Kale kwamba Yesu ndiye Kristo. Baadhi ya Wayahudi na Wayunani wakaamini, lakini ilimlazimu Paulo kuondoka huko haraka kwa sababu ya upinzani mkubwa uliozuka humo.
Baada ya kufika Athene, Paulo alipata habari kutoka kwa Timotheo kuwa ingawa walipata mateso, waumini wa Thesalonike walikuwa wamesimama imara. Paulo aliandika barua hii ili kuwatia moyo na kuwafariji waumini waliokuwa wachanga katika Kristo. Aliwaandikia ili kuimarisha imani yao kuhusu maisha yale Mkristo anapaswa kuishi, na pia kuhusu kurudi kwa Yesu. Yamkini waumini hawa walikuwa na wasiwasi kwamba Wakristo wenzao waliokuwa wamekufa hawangeweza kuufikia ufufuo wa wafu. Hivyo Paulo akawaandikia kuwahakikishia kwamba waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuka kwanza.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Kusudi
Kuwaimarisha Wakristo wa Thesalonike katika imani yao, na kuwapa hakikisho kuhusu kurudi kwa Yesu.
Mahali
Korintho.
Tarehe
Mnamo 51 B.K.
Wahusika Wakuu
Paulo, Timotheo na Silvano.
Wazo Kuu
Kuwatia waumini moyo kudumu katika utakatifu, na kuwahakikishia wale wanaoteswa kwamba Mungu yu pamoja nao na amewaahidi ushindi.
Mambo Muhimu
Paulo aliwaandikia Wathesalonike barua hii ili kuwatia moyo na kuwafariji katika Kristo, na pia kuimarisha imani yao katika misingi ya mafundisho ya Kristo.
Yaliyomo
Salamu na shukrani za Paulo (1:1‑10)
Huduma ya Paulo Thesalonike, na matukio tangu kuondoka Thesalonike (2:1–3:13)
Mwenendo na maisha ya kumcha Mungu (4:1‑12)
Kurudi kwake Bwana Yesu (4:13–5:11)
Maagizo ya mwisho, na hitimisho (5:12‑28).
Iliyochaguliwa sasa
1 Wathesalonike Utangulizi: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.