Wakolosai 4
4
1Ninyi mabwana, watendeeni watumwa wenu yaliyo haki na yanayostahili, mkitambua kwamba ninyi pia mnaye Bwana mbinguni.
Maagizo zaidi
2Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru. 3Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena neno lake, ili tupate kuitangaza siri ya Al-Masihi, ambayo kwa ajili yake nimefungwa. 4Ombeni ili nipate kuitangaza hiyo siri kwa udhahiri kama inipasavyo. 5Nendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. 6Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.
Salamu za mwisho
7Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtendakazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana Isa. 8Nimemtuma kwenu kwa lengo maalum la kuwafahamisha hali yetu, na pia awatie moyo. 9Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu.
10Aristarko aliye mfungwa pamoja nami anawasalimu, vivyo hivyo Marko, binamu yake Barnaba. (Mmeshapata maagizo yanayomhusu; akija kwenu, mpokeeni.) 11Isa aitwaye Yusto pia anawasalimu. Hawa peke yao ndio Wayahudi miongoni mwa watendakazi wenzangu kwa ajili ya ufalme wa Mungu, nao wamekuwa faraja kwangu.
12Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Al-Masihi Isa, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu, mkiwa wakamilifu na thabiti. 13Ninashuhudia kumhusu kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, na kwa ajili ya ndugu wa Laodikia na wale wa Hierapoli.
14Rafiki yetu mpendwa, Luka yule tabibu, pamoja na Dema, wanawasalimu.
15Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia, na pia Nimfa, pamoja na kundi la waumini wanaokutana katika nyumba yake.
16Baada ya barua hii kusomwa kwenu, hakikisheni kwamba inasomwa pia katika kundi la waumini wa Walaodikia. Nanyi pia msome barua inayotoka Laodikia.
17Mwambieni Arkipo hivi: “Hakikisha kuwa unakamilisha ile huduma uliyopokea katika Bwana Isa.”
18Mimi Paulo naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni minyororo yangu. Neema iwe nanyi.
Iliyochaguliwa sasa
Wakolosai 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.