Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 9

9
Samweli ampaka Sauli mafuta
1Kulikuwa na Mbenyamini mmoja, mtu maarufu, ambaye aliitwa Kishi mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia wa Benyamini. 2Alikuwa na mwana aliyeitwa Sauli, kijana aliyevutia sana, hakuna aliyelingana naye miongoni mwa Waisraeli; alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote.
3Basi punda wa Kishi baba yake Sauli walipotea, naye Kishi akamwambia mwanawe Sauli, “Mchukue mmoja wa watumishi mwende pamoja naye kuwatafuta punda.” 4Hivyo akapita katika nchi ya vilima ya Efraimu na katika eneo la Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakaendelea katika sehemu ya Shaalimu, lakini punda hawakuwa huko. Kisha wakapita katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwapata.
5Walipofika sehemu ya Sufu, Sauli akamwambia mtumishi aliyekuwa pamoja naye, “Njoo turudi, au baba yangu ataacha kufikiria kuhusu punda na kuanza kufadhaika kutuhusu.”
6Lakini mtumishi akajibu, “Tazama, katika mji huu yupo mtu wa Mungu, anayeheshimiwa sana na kila kitu asemacho kweli hutukia. Sasa na twende huko. Huenda atatuambia twende njia ipi.”
7Sauli akamwambia mtumishi wake, “Tukienda, tutampa nini huyo mtu? Chakula kimekwisha kwenye mifuko yetu. Hatuna zawadi ya kumpelekea huyo mtu wa Mungu. Je tuna nini?”
8Mtumishi akamjibu Sauli tena, akasema, “Tazama, nina fedha robo shekeli#9:8 Robo shekeli ni sawa na gramu 3.. Hiyo nitampa huyo mtu wa Mungu ili aweze kutuambia tutapitia njia ipi.” 9(Zamani katika Israeli, kama mtu alienda kuuliza neno kwa Mungu, angesema, “Njoo na twende kwa mwonaji,” kwa sababu nabii wa sasa alikuwa akiitwa mwonaji.)
10Sauli akamwambia mtumishi wake, “Vyema, njoo na twende.” Basi wakaenda mjini alipokuwa huyo mtu wa Mungu.
11Walipokuwa wakipanda mlima kwenda mjini, wakakutana na baadhi ya wasichana wakikuja kuchota maji, nao wakawauliza, “Je, mwonaji yuko?”
12Wakajibu, “Yuko, yu mbele yenu amewatangulia, sasa fanyeni haraka, ndiyo tu amekuja mjini kwetu leo, kwa kuwa watu wana dhabihu huko mahali pa juu pa kuabudia. 13Mara tu mwingiapo mjini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu pa kuabudia ili kula. Watu hawataanza kula hadi atakapofika, kwa sababu ni lazima kwanza yeye abariki dhabihu, ndipo wale walioalikwa watakapokula. Pandeni sasa, mtamkuta kwa wakati huu.”
14Wakapanda mjini, nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli alikuwa akija kuelekea walikoenda mahali pa juu pa kuabudia.
15Basi siku moja kabla Sauli hajaja, Mwenyezi Mungu alikuwa amemfunulia Samweli jambo hili: 16“Kesho wakati kama huu nitakupelekea mtu kutoka nchi ya Benyamini. Umpake mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Israeli; ndiye atakayewakomboa watu wangu na mkono wa Wafilisti. Nimewaangalia watu wangu, kwa kuwa kilio chao kimenifikia.”
17Samweli alipomwona Sauli, Mwenyezi Mungu akamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekuambia habari zake, kwamba yeye atawatawala watu wangu.”
18Sauli akamkaribia Samweli langoni na kumuuliza, “Tafadhali, je, unaweza kuniambia mahali nyumba ya mwonaji ilipo?”
19Samweli akamjibu Sauli, “Mimi ndiye mwonaji, panda utangulie mbele yangu hadi mahali pa juu pa kuabudia, kwa kuwa leo itakupasa kula pamoja nami na asubuhi nitakuruhusu uende na nitakuambia yale yote yaliyo moyoni mwako. 20Kuhusu wale punda uliowapoteza siku tatu zilizopita, usifadhaike kwa habari yao; wamepatikana. Ni kwa nani ambaye shauku yote ya Israeli imeelekea, kama si kwako na jamaa yote ya baba yako?”
21Sauli akajibu, “Je, mimi si Mbenyamini, kutoka kabila dogo kuliko yote ya Israeli, nao ukoo wangu si ndio mdogo kuliko koo zote za kabila la Benyamini? Kwa nini uniambie jambo kama hili?”
22Kisha Samweli akamleta Sauli na mtumishi wake ukumbini na kuwaketisha mahali pa heshima zaidi miongoni mwa wale waliokuwa wamealikwa; jumla yao walikuwa kama watu thelathini. 23Samweli akamwambia mpishi, “Leta ile sehemu ya nyama niliyokupa, ile niliyokuambia iweke kando.”
24Hivyo mpishi akachukua mguu pamoja na kile kilichokuwa juu yake akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, “Hiki ndicho ambacho kimewekwa kwa ajili yako. Ule, kwa sababu kilitengwa kwa ajili yako kwa tukio hili, tangu niliposema, ‘Nimewaalika wageni.’ ” Naye Sauli akala pamoja na Samweli siku ile.
25Baada ya kushuka kutoka mahali pa juu pa kuabudia na kufika mjini, Samweli alizungumza na Sauli juu ya dari ya nyumba yake. 26Walipoamka mapema alfajiri, Samweli akamwita Sauli darini, akamwambia, “Jiandae, nami nitakuaga uende zako.” Sauli alipokuwa tayari yeye na Samweli wakatoka nje pamoja. 27Walipokuwa wakiteremka kuelekea mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, “Mwambie mtumishi atangulie mbele yetu.” Naye mtumishi akafanya hivyo. “Subiri hapa kidogo ili nipate kukupa ujumbe kutoka kwa Mungu.”

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 9: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia