Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 8

8
Israeli waomba mfalme
1Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli. 2Mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba. 3Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki.
4Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama. 5Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.”
6Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwomba Mwenyezi Mungu. 7Naye Mwenyezi Mungu akamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao. 8Kama vile walivyofanya tangu siku nilipowapandisha kutoka Misri hadi siku hii ya leo; wakiniacha mimi na kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokufanyia wewe. 9Sasa wasikilize, lakini waonye sana, na uwafahamishe yale watakayotendewa na mfalme atakayewatawala.”
10Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote ya Mwenyezi Mungu. 11Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake. 12Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake ya vita. 13Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji. 14Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake. 15Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake. 16Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ng’ombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe. 17Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. 18Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, naye Mwenyezi Mungu hatawajibu.”
19Lakini watu wakakataa kumsikiliza Samweli wakasema, “Hapana! Tunataka mfalme wa kututawala. 20Kisha tutakuwa kama mataifa mengine yote, tukiwa na mfalme wa kutuongoza na kwenda mbele yetu na kutupigania vita vyetu.”
21Samweli aliposikia yote watu waliyosema, akarudia kuyasema mbele za Mwenyezi Mungu. 22Mwenyezi Mungu akamjibu, “Wasikilize na uwape mfalme.”
Kisha Samweli akawaambia Waisraeli, “Kila mmoja arudi mjini kwake.”

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 8: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia