1 Samweli 10
10
1Ndipo Samweli akachukua chupa ndogo ya mafuta na kuyamimina juu ya kichwa cha Sauli, akambusu, akisema, “Je, Mwenyezi Mungu hakukupaka mafuta uwe kiongozi juu ya urithi wake? 2Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli, huko Selsa kwenye mpaka wa Benyamini. Watakuambia, ‘Punda wale uliotoka kwenda kuwatafuta, wamekwisha kupatikana. Sasa baba yako ameacha kufikiri kuhusu punda na sasa ana hofu kukuhusu wewe. Anauliza, “Nitafanyaje kuhusu mwanangu?” ’
3“Kisha utaenda mbele kutoka hapa hadi uufikie mwaloni wa Tabori. Watu watatu wanaopanda kwenda kumwabudu Mungu huko Betheli watakutana nawe hapo. Mmoja atakuwa amechukua wana-mbuzi watatu, mwingine mikate mitatu, na mwingine kiriba cha divai. 4Watakusalimu na kukupa mikate miwili, ambayo utaipokea kutoka kwao.
5“Baada ya hayo utaenda Gibea ya Mungu, ambapo hapo kuna kambi ya Wafilisti. Unapokaribia mji utakutana na kundi la manabii wakiteremka kutoka mahali pa juu pa kuabudia wakiwa na vinubi, matari, filimbi na zeze vikipigwa mbele yao, nao watakuwa wakitoa unabii. 6Roho wa Mwenyezi Mungu atakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti. 7Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.
8“Tangulia kushuka mbele yangu hadi Gilgali. Hakika nami nitateremka nikujie ili kutoa dhabihu za sadaka za kuteketezwa na dhabihu za amani, lakini lazima ungoje kwa siku saba hata nitakapokujia na kukuambia likupasalo kufanya.”
Sauli afanywa mfalme
9Ikawa Sauli alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu aliubadilisha moyo wa Sauli, na ishara hizi zote zikatimizwa siku ile. 10Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao. 11Ikawa wale wote waliomfahamu hapo mwanzo walipomwona akitoa unabii pamoja na manabii, wakaulizana, “Ni nini hiki kilichomtokea mwana wa Kishi? Je, Sauli naye pia yumo miongoni mwa manabii?”
12Mtu mmoja ambaye aliishi huko akajibu, “Je, naye baba yao ni nani?” Basi ikawa mithali, kusema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?” 13Baada ya Sauli kumaliza kutoa unabii, alienda mahali pa juu pa kuabudia.
14Basi babaye mdogo akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Je, mlikuwa wapi?”
Akajibu, “Tulikuwa tukiwatafuta punda. Lakini tulipoona hawapatikani, tulienda kwa Samweli.”
15Babaye mdogo Sauli akasema, “Niambie Samweli amekuambia nini.”
16Sauli akajibu, “Alituhakikishia kwamba punda wamepatikana.” Lakini hakumwambia babaye mdogo kila kitu Samweli alichomwambia kuhusu ufalme.
17Samweli akawaita watu wa Israeli kuja kwa Mwenyezi Mungu huko Mispa, 18naye akawaambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Niliwatoa Israeli kutoka Misri, nami niliwaokoa toka nguvu za Misri na falme zote zilizowadhulumu.’ 19Lakini sasa mmemkataa Mungu wenu, ambaye anawaokoa toka katika maafa yenu yote na taabu zenu zote. Nanyi mmesema, ‘Hapana, tuteulie mfalme atutawale.’ Sasa basi, jihudhurisheni wenyewe mbele za Mwenyezi Mungu kwa makabila yenu na kwa koo zenu.”
20Samweli alipoyasogeza makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachaguliwa. 21Kisha akalisogeza mbele kabila la Benyamini, kufuatana na koo zao, nao ukoo wa Matri ukachaguliwa. Mwishoni Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipomtafuta, hakuonekana. 22Wakazidi kuuliza kwa Mwenyezi Mungu, “Je, huyo mtu amekwisha kufika hapa?”
Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, amejificha kwenye mizigo.”
23Wakakimbia na kumleta kutoka huko, naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote. 24Samweli akawaambia watu wote, “Je, mnamwona mtu ambaye Mwenyezi Mungu amemchagua? Hayupo aliye kama yeye miongoni mwa watu wote.”
Ndipo watu wakasema kwa sauti kuu, “Mfalme aishi maisha marefu.”
25Samweli akawaeleza watu madaraka ya ufalme. Akayaandika kwenye kitabu na kukiweka mbele za Mwenyezi Mungu. Kisha Samweli akawaruhusu watu kila mmoja aende nyumbani mwake.
26Sauli pia akaenda nyumbani mwake huko Gibea, akisindikizwa na watu hodari ambao Mungu alikuwa amegusa mioyo yao. 27Lakini baadhi ya watu wakorofi walisema, “Huyu mtu atawezaje kutuokoa?” Wakamdharau na wala hawakumletea zawadi. Lakini Sauli akakaa kimya.
Iliyochaguliwa sasa
1 Samweli 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.