Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 25

25
Daudi, Nabali na Abigaili
1Basi Samweli akafa, nao Waisraeli wote wakakusanyika na kumwombolezea; wakamzika nyumbani mwake huko Rama.
Kisha Daudi akateremka kwenye Jangwa la Parani. 2Mtu mmoja huko Maoni, aliyekuwa na makao huko Karmeli, alikuwa tajiri sana. Alikuwa na mbuzi elfu moja na kondoo elfu tatu, aliokuwa akiwakata manyoya huko Karmeli. 3Jina la mtu huyo lilikuwa Nabali, naye mkewe aliitwa Abigaili. Alikuwa mwanamke mwenye busara na mzuri wa sura, lakini mumewe, aliyekuwa wa ukoo wa Kalebu, alikuwa mwenye hasira na mchoyo katika utendaji wake.
4Daudi alipokuwa huko jangwani, akasikia kuwa Nabali alikuwa anakata kondoo manyoya. 5Basi akatuma vijana kumi na kuwaambia, “Pandeni kwa Nabali huko Karmeli, mkamsalimie kwa jina langu. 6Mwambieni: ‘Amani iwe kwako! Amani iwe kwako pamoja na wa nyumbani mwako! Pia amani iwe pamoja na vyote ulivyo navyo!
7“ ‘Nasikia kuwa huu ni wakati wa kukata kondoo manyoya. Wafugaji wako walipokuwa pamoja nasi, hatukuwatendea mabaya na wakati wote waliokuwa huko Karmeli hakuna chochote chao kilipotea. 8Waulize watumishi wako nao watakuambia. Kwa hiyo uwatendee wema vijana wangu, kwani tumekuja wakati wa furaha. Tafadhali wape watumishi wako na mwanao Daudi chochote kitakachokuja mkononi mwako kwa ajili yao.’ ”
9Watu wa Daudi walipofika wakampa Nabali ujumbe huu kwa jina la Daudi. Kisha wakangojea.
10Nabali akawajibu watumishi wa Daudi, “Huyu Daudi ni nani? Huyu mwana wa Yese ni nani? Watumishi wengi wanakimbia kutoka kwa bwana zao siku hizi. 11Kwa nini nichukue mkate wangu, maji yangu na nyama niliyochinja kwa ajili ya wakata manyoya wangu, na kuwapa watu ambao hakuna anayejua wanakotoka?”
12Watu wa Daudi wakageuka na kurudi. Walipofika, wakaarifu kila neno. 13Daudi akawaambia watu wake, “Jifungeni panga zenu!” Basi wakajifunga panga zao, naye Daudi akajifunga upanga wake. Watu kama mia nne hivi wakapanda pamoja na Daudi, na watu mia mbili wakabaki na vifaa.
14Mmoja wa watumishi akamwambia Abigaili, mkewe Nabali: “Daudi alituma wajumbe kutoka jangwani kumpa bwana wetu salamu zake, lakini akawatukana. 15Hata hivyo watu hawa walikuwa wema sana kwetu. Hawakututendea mabaya, na wakati wote tulipokuwa nje huko mashambani karibu nao, hatukupotewa na kitu chochote. 16Usiku na mchana walikuwa ukuta wa ulinzi wakati wote tulipokuwa tukichunga kondoo wetu karibu nao. 17Sasa fikiri juu ya jambo hili na uone unaweza kufanya nini, kwa sababu maafa yanakaribia juu ya bwana wetu na nyumba yake yote. Yeye ni mtu mwovu kiasi kwamba hakuna mtu awezaye kuzungumza naye.”
18Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate mia mbili, viriba viwili vya divai, kondoo watano waliochinjwa vipimo vitano vya bisi, vishada mia moja vya zabibu kavu, mikate mia mbili ya tini, akavipakia juu ya punda. 19Kisha akawaambia watumishi wake, “Tangulieni; mimi nitakuja nyuma yenu.” Lakini hakumwambia Nabali mumewe.
20Ikawa alipokuwa amepanda punda wake kwenye bonde la mlima, tazama, Daudi na watu wake wakawa wanateremka kumwelekea, naye akakutana nao. 21Daudi alikuwa amesema, “Ilikuwa ni kazi bure kuchunga kwangu kote mali ya huyu mtu huko jangwani hivi kwamba hakuna chochote chake kilichopotea. Yeye amenilipa baya kwa ajili ya wema. 22Mwenyezi Mungu na amwadhibu Daudi vikali zaidi, ikiwa kesho asubuhi nitambakizia mwanaume hata mmoja hai miongoni mwa watu wake wote!”
23Abigaili alipomwona Daudi, akashuka haraka kwenye punda wake, akamsujudia Daudi. 24Akamwangukia miguuni pake na kusema: “Bwana wangu, kosa hili na liwe juu yangu mwenyewe. Tafadhali mruhusu mtumishi wako aseme nawe. Sikia kile mtumishi wako atakachosema. 25Bwana wangu na asimjali huyo mtu mwovu Nabali. Yeye anafanana na jina lake; jina lake ni Mpumbavu, nao upumbavu huenda pamoja naye. Lakini kwangu mimi, mtumishi wako, sikuwaona hao watu waliotumwa na bwana wangu.
26“Basi sasa, bwana wangu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekuzuia kumwaga damu na kulipiza kisasi kwa mikono yako mwenyewe, hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na kama uishivyo, adui zako na wote wanaokusudia kumdhuru bwana wangu wawe kama Nabali. 27Nayo zawadi hii ambayo mtumishi wako amemletea bwana wangu, wapewe watu wanaofuatana nawe. 28Tafadhali samehe kosa la mtumishi wako, kwa kuwa Mwenyezi Mungu kwa hakika ataifanya imara nyumba ya ufalme kwa bwana wangu, kwa sababu anapigana vita vya Mwenyezi Mungu. 29Hata ingawa kuna mtu anayekufuatia ili akuue, usiruhusu baya lolote kuonekana kwako siku zote za maisha yako, uhai wa bwana wangu utafungwa salama kwenye furushi la walio hai na Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Lakini uhai wa adui zako utavurumishwa kama vile jiwe kutoka kombeo. 30Mwenyezi Mungu atakapokuwa ameshamtendea bwana wangu kila kitu chema alichoahidi kumhusu na kumweka kuwa kiongozi wa Israeli, 31bwana wangu hatakuwa na dhamiri inayolemewa na mzigo kwa kumwaga damu kusiko na sababu, au kujilipizia kisasi yeye mwenyewe. Mwenyezi Mungu atakapomletea bwana wangu mafanikio, umkumbuke mtumishi wako.”
32Daudi akamwambia Abigaili, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aliyekutuma kunilaki leo. 33Ubarikiwe kwa uamuzi wako mzuri na kwa kunizuia nisimwage damu leo na kulipiza kisasi kwa mikono yangu. 34La sivyo, hakika kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye amenizuia nisiwadhuru, kama usingekuja haraka kunilaki, hakuna mwanaume hata mmoja wa Nabali angeachwa hai kufikia mapambazuko.”
35Ndipo Daudi akapokea kutoka mkononi mwake kile alichokuwa amemletea, naye akasema, “Nenda nyumbani mwako kwa amani; nimesikia maneno yako na kukujalia ombi lako.”
36Abigaili alipoenda kwa Nabali, alikuwa ndani ya nyumba yake akifanya karamu kama ile ya mfalme. Naye alikuwa ana furaha nyingi, akiwa amelewa sana. Kwa hiyo Abigaili hakumwambia mumewe kitu chochote hadi asubuhi yake. 37Basi asubuhi, ulevi ulipokuwa umemtoka Nabali, mkewe akamwambia mambo yote, nao moyo wake ukazimia, akawa kama jiwe. 38Baada ya siku kumi, Mwenyezi Mungu akampiga Nabali, naye akafa.
39Daudi aliposikia kwamba Nabali amekufa, akasema, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, ambaye amenitetea dhidi ya Nabali kwa kuwa alinitendea kwa dharau. Amemzuia mtumishi wake asitende mabaya na Mwenyezi Mungu ameuleta ubaya wa Nabali juu ya kichwa chake mwenyewe.”
Kisha Daudi akatuma ujumbe kwa Abigaili kumwomba awe mke wake. 40Watumishi wa Daudi wakaenda Karmeli na kumwambia Abigaili, wakisema, “Daudi ametutuma kwako kukuchukua uwe mkewe.”
41Akasujudu uso wake ukielekea chini, akasema, “Mjakazi wako yuko hapa, tayari kuwatumikia na kuwanawisha miguu watumishi wa bwana wangu.” 42Abigaili akainuka kwa haraka, akapanda punda wake, akihudumiwa na wajakazi wake watano, akaenda pamoja na wajumbe wa Daudi, naye akawa mkewe. 43Pia Daudi alikuwa amemwoa Ahinoamu wa Yezreeli, wote wawili wakawa wake zake. 44Lakini Sauli alikuwa amemwoza Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi, kwa Palti mwana wa Laishi, kutoka Galimu.

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 25: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia