Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 26

26
Daudi amwacha Sauli hai tena
1Hao Wazifu wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kinachotazamana na Yeshimoni?”
2Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na wapiganaji wake elfu tatu wa Israeli waliochaguliwa, ili kumtafuta Daudi huko. 3Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko, 4Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili.
5Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali ambapo Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka.
6Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?”
Abishai akajibu, “Nitaenda pamoja nawe.”
7Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli.
8Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome hadi ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.”
9Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu na asiwe na hatia?” 10Daudi akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, Mwenyezi Mungu mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au ataenda vitani na kuangamia. 11Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.”
12Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito.
13Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima, mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao. 14Daudi akapaza sauti kwa jeshi na kwa Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?”
Abneri akajibu, “Nani wewe unayemwita mfalme?”
15Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako. 16Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?”
17Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?”
Daudi akajibu, “Naam, hiyo ndiyo, bwana wangu mfalme.” 18Pia akaongeza, “Kwa nini bwana wangu anamfuatia mtumishi wake? Nimefanya nini, nalo kosa langu ni lipi nililolifanya niwe na hatia? 19Sasa mfalme bwana wangu na asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama Mwenyezi Mungu amekuchochea dhidi yangu, basi yeye na aipokee sadaka yangu. Lakini kama ni wanadamu waliofanya hivyo, walaaniwe mbele za Mwenyezi Mungu! Wao sasa wamenifukuza kutoka sehemu yangu katika urithi wa Mwenyezi Mungu wangu wakisema, ‘Nenda ukatumikie miungu mingine.’ 20Basi usiache damu yangu imwagike kwenye ardhi mbali na uso wa Mwenyezi Mungu. Mfalme wa Israeli ametoka kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware katika milima.”
21Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.”
22Daudi akajibu, “Mkuki wa mfalme uko hapa. Mmoja wa vijana wako na avuke kuuchukua. 23Mwenyezi Mungu humlipa kila mtu kwa ajili ya haki yake na uaminifu wake. Mwenyezi Mungu alikutia katika mikono yangu leo, lakini sikuinua mkono wangu juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. 24Kwa hakika kama vile maisha yako yalivyokuwa ya thamani kwangu leo, vivyo hivyo maisha yangu na yawe na thamani kwa Mwenyezi Mungu na kuniokoa kutoka taabu zote.”
25Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Mwanangu Daudi na ubarikiwe; utafanya mambo makubwa na hakika utashinda.”
Basi Daudi akaenda zake, naye Sauli akarudi nyumbani.

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 26: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia