Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 24

24
Daudi amwacha Sauli hai
1Baada ya Sauli kurudi kuwafuatia Wafilisti, akaambiwa kwamba, “Daudi yuko katika Jangwa la En-Gedi.” 2Basi Sauli akachukua vijana wenye uwezo elfu tatu kutoka Israeli yote kwenda kumtafuta Daudi na watu wake karibu na Majabali ya Mbuzi-Mwitu.
3Akaja kwenye mazizi ya kondoo kando ya njia, hapo palikuwa na pango, na Sauli akaingia ndani kujipumzisha. Daudi na watu wake walikuwa wamo mle pangoni kwa ndani zaidi. 4Watu wa Daudi wakasema, “Hii ndiyo siku aliyonena Mwenyezi Mungu akikuambia, ‘Nitamtia adui yako mikononi mwako ili wewe umtendee utakavyo.’ ” Basi Daudi akanyemelea bila kuonekana na kukata upindo wa joho la Sauli.
5Baada ya hilo, dhamiri ya Daudi ikataabika kwa kukata upindo wa joho la Sauli. 6Akawaambia watu wake, “Mwenyezi Mungu na apishie mbali nisije nikafanya jambo kama hilo kwa bwana wangu, yeye ambaye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu, au kuinua mkono wangu dhidi yake; kwani yeye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.” 7Kwa maneno haya Daudi akawaonya watu wake na hakuwaruhusu wamshambulie Sauli. Naye Sauli akaondoka pangoni na kwenda zake.
8Ndipo Daudi naye akatoka pangoni na kumwita Sauli akisema, “Mfalme, bwana wangu!” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama na kumsujudia, uso wake ukigusa chini. 9Akamwambia Sauli, “Kwa nini unasikiliza wakati watu wanapokuambia, ‘Daudi amenuia kukudhuru’? 10Leo umeona kwa macho yako mwenyewe jinsi Mwenyezi Mungu alivyokutia mikononi mwangu huko pangoni. Watu wengine walisisitiza nikuue, lakini nilikuacha, nikisema, ‘Sitainua mkono wangu dhidi ya bwana wangu, kwa sababu yeye ni mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu.’ 11Tazama, baba yangu, ona kipande hiki cha joho lako mkononi mwangu! Nilikata upindo wa joho lako lakini sikukuua. Basi ujue na kutambua kuwa sina hatia ya kutenda mabaya wala kuasi. Wewe sijakukosea, lakini wewe unaniwinda mimi ili kuniua. 12Mwenyezi Mungu na ahukumu kati yangu na wewe. Naye Mwenyezi Mungu alipize mabaya unayonitendea, lakini mkono wangu hautakugusa. 13Kama msemo wa kale usemavyo, ‘Kutoka kwa watenda maovu hutoka matendo maovu,’ kwa hiyo mkono wangu hautakugusa wewe.
14“Je, mfalme wa Israeli ametoka dhidi ya nani? Ni nani unayemfuatia? Je, ni mbwa mfu? Ni kiroboto? 15Mwenyezi Mungu na awe mwamuzi wetu, yeye na aamue kati yetu. Yeye na anitetee shauri langu; anihesabie haki kwa kuniokoa mkononi mwako.”
16Daudi alipomaliza kusema haya, Sauli akamuuliza, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Ndipo Sauli akalia kwa sauti kuu. 17Akamwambia Daudi, “Wewe ni mwenye haki kuliko mimi; umenitendea mema, lakini mimi nimekutendea mabaya. 18Sasa umeniambia kuhusu mema uliyonitendea. Mwenyezi Mungu alinitia mikononi mwako, lakini wewe hukuniua. 19Je, mtu ampatapo adui yake, humwacha aende zake bila kumdhuru? Mwenyezi Mungu na akulipe mema kwa jinsi ulivyonitenda leo. 20Ninajua kwamba hakika utakuwa mfalme na kwamba ufalme wa Israeli utakuwa imara mikononi mwako. 21Sasa niapie kwa Mwenyezi Mungu kwamba hutakatilia mbali uzao wangu wala kulifuta jina langu kutoka jamaa ya baba yangu.”
22Basi Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akarudi zake nyumbani, lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 24: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia