Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 23

23
Daudi aokoa Keila
1Daudi alipoambiwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila, nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,” 2akauliza kwa Mwenyezi Mungu, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?”
Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uuokoe Keila.”
3Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Je, si zaidi tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!”
4Daudi akauliza kwa Mwenyezi Mungu tena, naye Mwenyezi Mungu akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.” 5Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila. 6Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kizibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila.
Sauli amfuata Daudi
7Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa ameenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.” 8Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi.
9Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kizibau.” 10Daudi akasema, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu. 11Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atateremka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.”
Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, atashuka.”
12Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?”
Naye Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.”
13Basi Daudi na watu wake wapatao mia sita wakaondoka Keila, wakawa wanaenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakuenda huko.
14Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku Sauli aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mkononi mwake.
15Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue. 16Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu. 17Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.” 18Wote wawili wakafanya agano mbele za Mwenyezi Mungu. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi.
19Basi Wazifu wakakwea kwa Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu katika ngome huko Horeshi, katika kilima cha Hakila, kusini mwa Yeshimoni? 20Sasa, ee mfalme, uteremke wakati wowote unapoona vyema kufanya hivyo, sisi tutawajibika kumkabidhi kwa mfalme.”
21Sauli akajibu, “Mwenyezi Mungu awabariki kwa kunifikiria. 22Nendeni mkafanye maandalizi zaidi. Mkajue mahali Daudi huenda mara kwa mara, na nani amepata kumwona huko. Wananiambia yeye ni mjanja sana. 23Jueni kila mahali anapojificha, kisha mrudi na kunipa taarifa kamili. Nami nitaenda pamoja nanyi; kama atakuwa katika eneo hilo, nitamsaka miongoni mwa koo zote za Yuda.”
24Basi wakaondoka na kwenda hadi Zifu wakimtangulia Sauli. Naye Daudi na watu wake walikuwa katika Jangwa la Maoni, katika Araba kusini mwa Yeshimoni. 25Sauli na watu wake wakaanza msako, naye Daudi alipoelezwa hili, akateremka hadi mwambani na kukaa katika Jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hili, akaenda katika Jangwa la Maoni akimfuata Daudi.
26Sauli alikuwa akienda upande mmoja wa mlima, naye Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima, wakiharakisha kumkimbia Sauli. Sauli na majeshi yake walipokaribia kumkamata Daudi na watu wake, 27mjumbe alikuja kwa Sauli, akisema, “Njoo haraka! Wafilisti wanaishambulia nchi.” 28Ndipo Sauli akarudi akaacha kumfuata Daudi na kwenda kukabiliana na Wafilisti. Ndiyo sababu wanaiita sehemu hii Sela-Hamalekothi#23:28 maana yake Mwamba wa Kutengana. 29Naye Daudi akakwea kutoka huko na kuishi katika ngome za En-Gedi.

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 23: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia