Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Petro 2

2
Jiwe lililo hai na watu waliochaguliwa
1Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna. 2Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu, 3ikiwa kweli mmeonja kwamba Bwana Isa ni mwema.
4Mnapokuja kwake, yeye aliye Jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu bali kwa Mungu ni teule na la thamani kwake, 5ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mnajengwa kuwa nyumba ya kiroho, ili mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kupitia kwa Isa Al-Masihi. 6Kwa maana imeandikwa katika Maandiko:
“Tazama, naweka katika Sayuni,
jiwe la pembeni teule lenye thamani,
na yeyote atakayemwamini
hataaibishwa kamwe.”#2:6 Isaya 28:16
7Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hili ni la thamani. Lakini kwao wasioamini,
“Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni,”#2:7 Zaburi 118:22
8tena,
“Jiwe lenye kuwafanya watu wajikwae,
na mwamba wa kuwaangusha.”#2:8 Isaya 8:14
Wanajikwaa kwa sababu hawakulitii lile neno, kama walivyowekewa tangu zamani.
9Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. 10Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.
11Wapendwa, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. 12Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.
Kuwatii wenye mamlaka
13Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu: Awe ni mfalme kwani ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi, 14au wawe maafisa aliowaweka. Kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale wanaotenda mema. 15Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema myanyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu. 16Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu. 17Mheshimuni kila mtu ipasavyo, wapendeni waumini wote, mcheni Mungu, mpeni heshima mfalme.
18Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu kwa heshima yote, si wale mabwana walio wema na wapole peke yao, bali pia wale walio wakali. 19Kwa maana ni jambo la sifa kama mtu akivumilia anapoteswa kwa uonevu kwa ajili ya Mungu. 20Kwani ni faida gani kwa mtu kustahimili anapopigwa kwa sababu ya makosa yake? Lakini mkiteswa kwa sababu ya kutenda mema, nanyi mkastahimili, hili ni jambo la kusifiwa mbele za Mungu.
Mfano wa mateso ya Al-Masihi
21Ninyi mliitwa kwa ajili ya haya, kwa sababu Al-Masihi naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake.
22“Yeye hakutenda dhambi,
wala hila haikuonekana kinywani mwake.”#2:22 Isaya 53:9
23Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki. 24Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, na tupate kuishi katika haki. Kwa majeraha yake, ninyi mmeponywa.#2:24 Isaya 53:5 25Kwa maana mlikuwa mmepotea kama kondoo,#2:25 Isaya 53:6 lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.

Iliyochaguliwa sasa

1 Petro 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Petro 2

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha