1 Petro 1
1
Salamu
1Petro, mtume wa Isa Al-Masihi.
Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, jimbo la Asia, na Bithinia. 2Ni ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba#1:2 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi kulingana na alivyotangulia kuwajua, kupitia kwa kazi ya utakaso wa Roho wa Mungu, katika utiifu kwa Isa Al-Masihi na kunyunyiziwa damu yake.
Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi.
Tumaini lenye uzima
3Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi! Kwa rehema zake kuu, ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima, kupitia kwa kufufuka kwa Isa Al-Masihi kutoka kwa wafu, 4ili tuupate urithi usioangamia, usioharibika, na usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. 5Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kupitia kwa imani, hadi utakapokuja ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. 6Katika haya yote mnafurahi sana, ijapokuwa kwa muda mfupi sasa mmehuzunishwa kwa majaribu ya aina nyingi. 7Haya yamewajia ili imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo ingawa inasafishwa kwa moto, ionekane kuwa halisi, na imalizie kwa sifa, utukufu na heshima Isa Al-Masihi atakapodhihirishwa. 8Ijapokuwa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha yenye utukufu na isiyoelezeka. 9Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.
10Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewafikia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa. 11Walijaribu kujua ni wakati upi na ni mazingira yapi ambayo Roho wa Al-Masihi, aliyekuwa ndani yao, alionesha alipotabiri mateso ya Al-Masihi na utukufu ambao ungefuata. 12Walifunuliwa kwamba walikuwa wanawahudumia ninyi, bali si wao wenyewe, waliponena kuhusu mambo hayo. Mmeambiwa mambo haya sasa na wale waliowahubiria Injili kwa Roho wa Mungu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.
Mwito wa kuishi maisha matakatifu
13Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Isa Al-Masihi atakapodhihirishwa. 14Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. 15Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. 16Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”#1:16 Walawi 11:44, 45; 19:2
17Kwa kuwa mnamlilia Baba anayehukumu kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, kaeni kama wageni wakati wenu duniani, mkiogopa na kumcha Mungu. 18Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa, ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu. Hamkukombolewa kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, 19bali mlikombolewa kwa damu ya thamani ya Al-Masihi, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. 20Yeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika nyakati hizi za mwisho kwa ajili yenu. 21Kupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu.
22Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli hata mkawa na upendo wa ndugu usio na unafiki, basi pendaneni kwa dhati kutoka moyoni. 23Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu inayoharibika, bali kwa mbegu isiyoharibika, kupitia kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele. 24Maana,
“Wanadamu wote ni kama majani,
nao utukufu wao wote ni kama maua ya kondeni;
majani hunyauka na maua huanguka,
25lakini neno la Mwenyezi Mungu ladumu milele.”#1:25 Isaya 40:6-8
Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.
Iliyochaguliwa sasa
1 Petro 1: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.