1 Wafalme 2:12-25
1 Wafalme 2:12-25 NENO
Kwa hiyo Sulemani akaketi kwenye kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana. Basi Adoniya, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Sulemani. Bathsheba akamuuliza, “Je, umekuja kwa amani?” Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.” Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.” Akajibu, “Unaweza kulisema.” Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, na ufalme umeenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.” Bathsheba akasema, “Unaweza kuliomba.” Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Sulemani, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.” Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.” Bathsheba alipoenda kwa Mfalme Sulemani kuzungumza naye kwa ajili ya Adoniya, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akamketisha mkono wake wa kuume. Bathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.” Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.” Akasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adoniya.” Mfalme Sulemani akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi Mshunami, kwa ajili ya Adoniya? Mwombee na ufalme pia kwani yeye ni ndugu yangu mkubwa: naam, kwa ajili yake, na kwa ajili ya kuhani Abiathari, na Yoabu mwana wa Seruya!” Mfalme Sulemani akaapa kwa Mwenyezi Mungu, akasema: “Mungu na aniadhibu vikali zaidi ikiwa Adoniya hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili! Basi sasa, hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu, naye amenipa ufalme wa kudumu kama alivyoahidi, Adoniya atauawa leo!” Hivyo Mfalme Sulemani akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa.