Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 2:12-25

1 Wafalme 2:12-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Solomoni akaketi katika kiti cha enzi mahali pa Daudi, baba yake; na ufalme wake ukaimarika. Baadaye, Adoniya mwana wa Hagithi, alimwendea Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamwuliza, “Je, unakuja kwa amani?” Adoniya akamjibu, “Ndiyo, nakuja kwa amani. Ila, nina jambo moja tu la kukuambia.” Bathsheba akamwambia, “Sema tu.” Adoniya akamwambia, “Unajua kwamba mimi ningalikuwa mfalme, na hata Israeli yote ilikuwa inanitazamia niwe mfalme. Lakini, mambo yakageuka na ndugu yangu akanipindua, kwani hayo ndio yaliyokuwa mapenzi yake Mwenyezi-Mungu. Sasa, ninalo ombi moja tu ambalo nakusihi usinikatalie.” Bathsheba akamwambia, “Sema tu.” Naye akasema, “Tafadhali, nakusihi umwombe mfalme Solomoni aniruhusu nimchukue Abishagi, yule Mshunami, awe mke wangu, kwa maana najua hatakukatalia wewe.” Bathsheba akamwambia, “Sawa; nitazungumza na mfalme kwa niaba yako.” Basi, Bathsheba akamwendea mfalme Solomoni kumweleza ombi la Adoniya. Mfalme akainuka kwenda kumlaki mama yake, akamwinamia. Halafu, akaketi katika kiti chake cha enzi, akaagiza mama yake aletewe kiti; naye akakaa upande wa kulia wa mfalme. Bathsheba akasema, “Nina ombi dogo tafadhali ulikubali, na ninakuomba usinikatalie.” Mfalme akamwambia, “Sema ombi lako mama yangu, kwa sababu sitakukatalia.” Naye akasema, “Mruhusu ndugu yako Adoniya amwoe Abishagi, huyo Mshunami.” Mfalme Solomoni akamwuliza mama yake, “Kwa nini unataka nimpe Abishagi? Hii ni sawa kabisa na kumtakia ufalme wangu! Kumbuka ya kwamba yeye ni kaka yangu mkubwa, na isitoshe, kuhani Abiathari na jemadari Yoabu mwana wa Seruya, wako upande wake!” Hapo mfalme Solomoni akaapa kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akisema, “Mungu na aniulie mbali ikiwa Adoniya hatakufa kwa sababu ya kutoa ombi hili! Sasa basi, kwa jina la Mwenyezi-Mungu aliye hai, aliyeniweka na kuniimarisha katika ufalme wa baba yangu Daudi, na aliyetimiza ahadi yake, akanipa enzi mimi na wazawa wangu, naapa kwamba hivi leo Adoniya atakufa!” Ndipo mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada; naye akamwendea Adoniya, akamuua.

1 Wafalme 2:12-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akaja kwa Bathsheba mamaye Sulemani. Naye akasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akajibu, Kwa amani. Tena akasema, Nina jambo ninalotaka kukuambia. Naye akamwambia, Sema. Basi akasema, Wajua ya kwamba ufalme ulikuwa wangu, na Israeli wote wakaniwekea nyuso zao ili mimi nimiliki; lakini sasa ufalme umegeuka kuwa wake ndugu yangu; kwa maana ulikuwa wake kutoka kwa BWANA. Basi sasa nina haja moja ninayokuomba, usinikataze hiyo. Naye akamwambia, Sema. Akasema, Nakusihi nena na Sulemani, mfalme (kwa kuwa hawezi kukukatalia neno), kwamba anioze Abishagi, Mshunami. Naye Bathsheba akasema, Vema; nitasema na mfalme kwa ajili yako. Basi Bathsheba akaingia kwa mfalme Sulemani, aseme naye kwa ajili ya Adonia. Naye mfalme akainuka kwenda kumlaki, akamwinamia, akaketi katika kiti chake cha enzi; kisha akaagiza awekewe kiti cha enzi mamaye mfalme; naye akaketi mkono wake wa kulia. Ndipo akasema, Haja moja ndogo nakuomba; usinikatalie. Mfalme akamwambia, Omba, mama; kwa kuwa siwezi kukukatalia neno. Naye akasema, Nataka Adonia, ndugu yako, aozwe Abishagi, Mshunami. Mfalme Sulemani akajibu, akamwambia mamaye, Na mbona wamtakia Adonia Abishagi, Mshunami? Umtakie na ufalme pia; kwa kuwa yeye ni ndugu yangu mkubwa; naam, umtakie yeye, na Abiathari kuhani, na Yoabu mwana wa Seruya. Ndipo mfalme Sulemani akaapa kwa BWANA, akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, isipokuwa Adonia amenena neno hili juu ya uhai wake mwenyewe. Basi kwa hiyo, BWANA aishivyo, aliyenithibitisha na kunikalisha katika kiti cha enzi cha Daudi baba yangu, akanifanyia nyumba, kama alivyoahidi, hakika atauawa leo hivi Adonia. Mfalme Sulemani akatuma kuwa jambo hilo liwe mkononi mwa Benaya mwana wa Yehoyada: naye akampiga, hata akafa.

1 Wafalme 2:12-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akaja kwa Bath-sheba mamaye Sulemani. Naye akasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akajibu, Kwa amani. Tena akasema, Nina shauri ninalotaka kukuambia. Naye akamwambia, Sema. Basi akasema, Wajua ya kwamba ufalme ulikuwa wangu, na Israeli wote wakaniwekea nyuso zao ili nimiliki mimi; walakini sasa ufalme umegeuka kuwa wake ndugu yangu; kwa maana ulikuwa wake kutoka kwa BWANA. Basi sasa nina haja moja ninayokuomba, usinikataze hiyo. Naye akamwambia, Sema. Akasema, Nena, nakusihi, na Sulemani, mfalme, (kwa kuwa hawezi kukukataza neno), kwamba anioze Abishagi, Mshunami. Naye Bath-sheba akasema, Vema; nitasema na mfalme kwa ajili yako. Basi Bath-sheba akaingia kwa mfalme Sulemani, aseme naye kwa ajili ya Adonia. Naye mfalme akainuka kwenda kumlaki, akamwinamia, akaketi katika kiti chake cha enzi; kisha akaagiza awekewe kiti cha enzi mamaye mfalme; naye akaketi mkono wake wa kuume. Ndipo akasema, Haja moja ndogo nakuomba; usinikataze. Mfalme akamwambia, Omba, mama; kwa kuwa siwezi kukukataza neno. Naye akasema, Nataka Adonia, ndugu yako, aozwe Abishagi, Mshunami. Akajibu mfalme Sulemani akamwambia mamaye, Na mbona wamtakia Adonia Abishagi, Mshunami? Umtakie na ufalme pia; kwa kuwa yeye ni ndugu yangu mkubwa; naam, umtakie yeye, na Abiathari kuhani, na Yoabu mwana wa Seruya. Ndipo mfalme Sulemani akaapa kwa BWANA, akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, isipokuwa Adonia amenena neno hili juu ya uhai wake mwenyewe. Basi kwa hiyo, BWANA aishivyo, aliyenithibitisha na kunikalisha katika kiti cha enzi cha Daudi baba yangu, akanifanyia nyumba, kama alivyoahidi, hakika atauawa leo hivi Adonia. Mfalme Sulemani akatuma kwa mkono wa Benaya mwana wa Yehoyada: naye akampiga, hata akafa.

1 Wafalme 2:12-25 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Kwa hiyo Sulemani akaketi kwenye kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana. Basi Adoniya, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Sulemani. Bathsheba akamuuliza, “Je, umekuja kwa amani?” Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.” Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.” Akajibu, “Unaweza kulisema.” Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, na ufalme umeenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.” Bathsheba akasema, “Unaweza kuliomba.” Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Sulemani, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.” Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.” Bathsheba alipoenda kwa Mfalme Sulemani kuzungumza naye kwa ajili ya Adoniya, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akamketisha mkono wake wa kuume. Bathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.” Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.” Akasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adoniya.” Mfalme Sulemani akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi Mshunami, kwa ajili ya Adoniya? Mwombee na ufalme pia kwani yeye ni ndugu yangu mkubwa: naam, kwa ajili yake, na kwa ajili ya kuhani Abiathari, na Yoabu mwana wa Seruya!” Mfalme Sulemani akaapa kwa Mwenyezi Mungu, akasema: “Mungu na aniadhibu vikali zaidi ikiwa Adoniya hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili! Basi sasa, hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu, naye amenipa ufalme wa kudumu kama alivyoahidi, Adoniya atauawa leo!” Hivyo Mfalme Sulemani akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa.