1 Wafalme 2
2
Maagizo ya Daudi kwa Sulemani
1Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Sulemani agizo.
2Akasema, “Ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jioneshe kuwa mwanaume, 3shika lile Mwenyezi Mungu, Mungu wako, analokuagiza: Nenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote utakapoenda, 4na ili Mwenyezi Mungu aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’
5“Sasa wewe mwenyewe unafahamu lile Yoabu mwana wa Seruya alilonitendea, lile alilofanya kwa majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua, akimwaga damu yao wakati wa amani kama vile ni kwenye vita, tena akaipaka damu ile kwenye mkanda uliokuwa kiunoni mwake na viatu alivyovaa miguuni mwake. 6Mtendee kwa kadiri ya hekima yako, lakini usiache kichwa chake chenye mvi kishukie kaburi kwa amani.
7“Lakini uwaoneshe wema wana wa Barzilai wa Gileadi na uwaruhusu wawe miongoni mwa wale walao mezani pako. Walisimama nami nilipomkimbia ndugu yako Absalomu.
8“Ukumbuke, unaye Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini kutoka Bahurimu, aliyenilaani kwa laana kali siku niliyoenda Mahanaimu. Aliposhuka kunilaki huko Yordani, nilimwapia kwa Mwenyezi Mungu: ‘Sitakuua kwa upanga!’ 9Lakini sasa, usidhani kwamba hana hatia. Wewe ni mtu wa hekima, utajua la kumtendea. Zishushe mvi zake kaburini kwa damu.”
10Kisha Daudi akalala na baba zake, naye akazikwa katika Mji wa Daudi. 11Daudi alikuwa ametawala Israeli miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na tatu. 12Kwa hiyo Sulemani akaketi kwenye kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana.
Kiti cha ufalme cha Sulemani chaimarishwa
13Basi Adoniya, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Sulemani. Bathsheba akamuuliza, “Je, umekuja kwa amani?”
Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.” 14Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.”
Akajibu, “Unaweza kulisema.”
15Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, na ufalme umeenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwa Mwenyezi Mungu. 16Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.”
Bathsheba akasema, “Unaweza kuliomba.”
17Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Sulemani, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.”
18Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.”
19Bathsheba alipoenda kwa Mfalme Sulemani kuzungumza naye kwa ajili ya Adoniya, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akamketisha mkono wake wa kuume.
20Bathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.”
Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.”
21Akasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adoniya.”
22Mfalme Sulemani akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi Mshunami, kwa ajili ya Adoniya? Mwombee na ufalme pia kwani yeye ni ndugu yangu mkubwa: naam, kwa ajili yake, na kwa ajili ya kuhani Abiathari, na Yoabu mwana wa Seruya!”
23Mfalme Sulemani akaapa kwa Mwenyezi Mungu, akasema: “Mungu na aniadhibu vikali zaidi ikiwa Adoniya hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili! 24Basi sasa, hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu, naye amenipa ufalme wa kudumu kama alivyoahidi, Adoniya atauawa leo!” 25Hivyo Mfalme Sulemani akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa.
26Mfalme akamwambia kuhani Abiathari, “Nenda huko Anathothi katika mashamba yako. Wewe unastahili kufa, lakini sitakuua sasa, kwa sababu ulilichukua Sanduku la Bwana Mungu Mwenyezi mbele ya Daudi baba yangu na ulishiriki taabu zote za baba yangu.” 27Hivyo Sulemani akamwondoa Abiathari kwenye ukuhani wa Mwenyezi Mungu, akilitimiza neno la Mwenyezi Mungu alilokuwa amenena huko Shilo kuhusu nyumba ya Eli.
28Habari zilipomfikia Yoabu, aliyekuwa amepanga njama na Adoniya, lakini sio na Absalomu, alikimbilia kwenye hema la Mwenyezi Mungu na kushika pembe za madhabahu. 29Mfalme Sulemani akaambiwa kuwa Yoabu amekimbilia kwenye hema la Mwenyezi Mungu naye alikuwa kando ya madhabahu. Basi Sulemani akamwagiza Benaya mwana wa Yehoyada: “Nenda ukamuue!”
30Ndipo Benaya akaingia kwenye hema la Mwenyezi Mungu na kumwambia Yoabu, “Mfalme anasema, ‘Toka nje!’ ”
Lakini akajibu, “La! Nitafia hapa hapa.”
Benaya akamwarifu mfalme, “Hivi ndivyo Yoabu alivyonijibu.”
31Kisha mfalme akamwamuru Benaya, “Fanya kama asemavyo. Muue na kumzika, ili uniondolee mimi na nyumba ya baba yangu dhambi ya damu isiyokuwa na hatia ile Yoabu aliyoimwaga. 32Mwenyezi Mungu atamlipiza kwa ajili ya damu aliyoimwaga, kwa sababu pasipo Daudi baba yangu kujua, aliwashambulia watu wawili na kuwaua kwa upanga. Wote wawili, Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda, walikuwa watu wazuri na wanyofu kuliko yeye. 33Hatia ya damu yao na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na wazao wake milele. Lakini kwa Daudi na uzao wake, nyumba yake na kiti chake cha ufalme, iwepo amani ya Mwenyezi Mungu milele.”
34Basi Benaya mwana wa Yehoyada akakwea, akamgonga na kumuua Yoabu, naye akazikwa katika shamba lake mwenyewe jangwani. 35Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada juu ya jeshi kwenye nafasi ya Yoabu, na kumweka kuhani Sadoki badala ya Abiathari.
36Kisha mfalme akatuma ujumbe kwa Shimei na kumwambia, “Ujijengee nyumba huko Yerusalemu uishi huko, lakini usiende mahali pengine popote. 37Siku utakayoondoka kuvuka Bonde la Kidroni, uwe na hakika utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.”
38Shimei akamjibu mfalme, “Ulilolisema ni jema. Mtumishi wako atatenda kama bwana wangu mfalme alivyosema.” Naye Shimei akakaa Yerusalemu kwa muda mrefu.
39Lakini baada ya miaka mitatu, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi, naye Shimei akaambiwa, “Watumwa wako wameenda Gathi.” 40Kwa ajili ya hili, Shimei akatandika punda wake, akaenda kwa Akishi huko Gathi kuwatafuta watumwa wake. Basi Shimei akaondoka na kuwarudisha watumwa wake kutoka Gathi.
41Sulemani alipoambiwa kuwa Shimei ametoka Yerusalemu na kwenda Gathi na amekwisha kurudi, 42mfalme akamwita Shimei na kumwambia, “Je, sikukuapiza kwa Mwenyezi Mungu na kukuonya kuwa, ‘Siku utakayoondoka kwenda mahali pengine popote, uwe na hakika utakufa’? Wakati ule uliniambia, ‘Ulilolisema ni jema. Nitatii!’ 43Kwa nini basi hukutunza kiapo chako kwa Mwenyezi Mungu na kutii amri niliyokupa?”
44Pia mfalme akamwambia Shimei, “Unajua moyoni mwako makosa yote uliyomtendea baba yangu Daudi. Sasa Mwenyezi Mungu atakulipiza kwa ajili ya mabaya yako uliyotenda. 45Lakini Mfalme Sulemani atabarikiwa, na kiti cha ufalme cha Daudi kitaimarishwa mbele za Mwenyezi Mungu milele.”
46Kisha mfalme akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka nje, akamgonga Shimei na kumuua.
Sasa ufalme ukawa umeimarika mikononi mwa Sulemani.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wafalme 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.