Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1

1
Adoniya ajitangaza mfalme
1Mfalme Daudi alipokuwa mzee umri ukiwa umesogea, hakuweza kupata joto hata walipomfunika kwa nguo. 2Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, “Turuhusu tumtafute mwanamwali bikira amhudumie mfalme na kumtunza. Anaweza kulala pembeni mwake ili bwana wetu mfalme apate joto.”
3Kisha wakatafuta katika Israeli yote ili kumpata msichana mzuri wa sura na wakampata Abishagi Mshunami, wakamleta kwa mfalme. 4Msichana huyo alikuwa mzuri sana wa sura. Akamtunza mfalme na kumhudumia, lakini mfalme hakufanya naye tendo la ndoa.
5Basi Adoniya mwana wa Hagithi akajigamba na kusema, “Mimi nitakuwa mfalme.” Hivyo akaweka tayari magari ya vita na wapanda farasi, pamoja na watu hamsini wa kumtangulia wakikimbia. 6(Baba yake hakuwa ameingilia na kumuuliza, “Kwa nini unafanya hivyo?” Alikuwa pia kijana mzuri sana wa sura, na alizaliwa baada ya Absalomu.)
7Adoniya akashauriana na Yoabu mwana wa Seruya, na kuhani Abiathari, nao wakamsaidia. 8Lakini kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada, nabii Nathani, Shimei, Rei na walinzi maalum wa Daudi hawakujiunga na Adoniya.
9Ndipo Adoniya akatoa dhabihu ya kondoo, ng’ombe na ndama walionona kwenye Jiwe la Zohelethi karibu na En-Rogeli. Akawaalika ndugu zake wote wana wa mfalme, na wanaume wote wa Yuda waliokuwa maafisa wa mfalme, 10lakini hakumwalika nabii Nathani, wala Benaya, wala walinzi maalum wa mfalme, wala ndugu yake Sulemani.
11Ndipo Nathani akamuuliza Bathsheba, mama yake Sulemani, “Je, hujasikia kwamba Adoniya mwana wa Hagithi, amekuwa mfalme pasipo bwana wetu Daudi kujua jambo hili? 12Sasa basi, acha nikushauri jinsi utakavyookoa uhai wako mwenyewe na uhai wa mwanao Sulemani. 13Ingia kwa Mfalme Daudi na umwambie, ‘Bwana wangu mfalme, je hukuniapia mimi mtumishi wako: “Hakika mwanao Sulemani atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme”? Kwa nini basi Adoniya amekuwa mfalme?’ 14Utakapokuwa ukizungumza na mfalme, nitaingia na kuthibitisha hayo uliyoyasema.”
15Hivyo Bathsheba akaenda kumwona mfalme chumbani mwake, ambapo Abishagi Mshunami alikuwa akimhudumia; naye mfalme alikuwa mzee sana. 16Bathsheba akainama na kusujudu, uso wake ukagusa chini mbele ya mfalme.
Mfalme akauliza, “Ni nini unachokitaka?”
17Akamwambia, “Bwana wangu, wewe mwenyewe uliniapia mimi mtumishi wako kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwamba: ‘Sulemani Mwanao atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme.’ 18Lakini sasa Adoniya amekuwa mfalme, nawe, bwana wangu mfalme huna habari kuhusu jambo hilo. 19Ametoa dhabihu idadi kubwa ya ng’ombe, ndama walionona na kondoo, naye amewaalika wana wa mfalme wote, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini hakumwalika Sulemani mtumishi wako. 20Bwana wangu mfalme, macho ya Israeli yote yanakutazama wewe wajue kutoka kwako kuwa ni nani atakayeketi kwenye kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake. 21Kama sivyo, mara tu bwana wangu mfalme atakapopumzishwa pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutatendewa kama wahalifu.”
22Alipokuwa angali anazungumza na mfalme, nabii Nathani akafika. 23Wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Kisha akaenda mbele ya mfalme na kumsujudia hadi uso wake ukagusa chini.
24Nathani akasema, “Je, bwana wangu mfalme, umetangaza kuwa Adoniya atakuwa mfalme baada yako na kwamba ataketi kwenye kiti chako cha ufalme? 25Leo ameshuka na kutoa dhabihu idadi kubwa ya ng’ombe, ndama walionona na kondoo. Amewaalika wana wote wa mfalme, jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari. Sasa hivi, wanakula na kunywa pamoja naye wakisema, ‘Aishi maisha marefu, Mfalme Adoniya!’ 26Lakini mimi mtumishi wako, na kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada, na mtumishi wako Sulemani hakutualika. 27Je, hili ni jambo ambalo bwana wangu mfalme amelifanya pasipo kuwajulisha watumishi wake ili wapate kujua ni nani atakayeketi kwenye kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake?”
Daudi amteua Sulemani kuwa mfalme
28Ndipo Mfalme Daudi akasema, “Mwite Bathsheba, aingie ndani.” Hivyo akaingia mbele ya mfalme na kusimama mbele yake.
29Ndipo mfalme akaapa: “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, ambaye ameniokoa kutoka kila taabu, 30hakika nitatekeleza leo kile nilichokuapia kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwanao Sulemani atakuwa mfalme baada yangu, naye ataketi kwenye kiti changu cha ufalme baada yangu.”
31Kisha Bathsheba akasujudu, uso wake ukigusa chini mbele ya mfalme, akasema, “Bwana wangu Mfalme Daudi na aishi milele!”
32Mfalme Daudi akasema, “Mwite kuhani Sadoki ndani, na nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Walipofika mbele ya mfalme, 33akawaambia: “Wachukueni watumishi wa bwana wenu pamoja nanyi na mkamkalishe mwanangu Sulemani juu ya nyumbu wangu mwenyewe, kisha mkamteremshe hadi Gihoni. 34Huko kuhani Sadoki na nabii Nathani wampake mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Pigeni tarumbeta na mpaze sauti, mkisema, ‘Mfalme Sulemani aishi maisha marefu!’ 35Kisha mtapanda pamoja naye, atakuja na kuketi kwenye kiti changu cha ufalme na kutawala baada yangu. Nimemweka atawale juu ya Israeli na Yuda.”
36Benaya mwana wa Yehoyada akamjibu mfalme, “Amen! Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu mfalme, na aamuru vivyo hivyo. 37Kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa na bwana wangu mfalme, vivyo hivyo na awe na Sulemani kukifanya kiti chake cha utawala kuwa kikuu kuliko kile cha bwana wangu Mfalme Daudi!”
38Hivyo kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi wakaenda na kumpandisha Sulemani juu ya nyumbu wa Mfalme Daudi, nao wakamsindikiza hadi Gihoni. 39Kuhani Sadoki akachukua pembe ya mafuta kutoka hema takatifu na kumtia Sulemani mafuta. Kisha wakapiga tarumbeta na watu wote wakapaza sauti wakisema, “Mfalme Sulemani aishi maisha marefu!” 40Na watu wote wakakwea wakimfuata, huku wakipiga filimbi na kushangilia sana, hata ardhi ikatikisika kwa ile sauti.
41Adoniya pamoja na wageni wote waliokuwa pamoja naye wakasikia sauti hiyo walipokuwa wakimalizia karamu yao. Waliposikia sauti ya tarumbeta, Yoabu akauliza, “Nini maana ya makelele haya yote katika mji?”
42Hata alipokuwa anaongea, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akafika. Adoniya akasema, “Ingia ndani. Mtu wa maana kama wewe ni lazima awe amelete habari njema.”
43Yonathani akamjibu, “La hasha! Mfalme Daudi bwana wetu amemfanya Sulemani kuwa mfalme. 44Mfalme ametuma pamoja naye kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, 45nao kuhani Sadoki na nabii Nathani wamempaka mafuta huko Gihoni kuwa mfalme. Kutoka hapo wamepanda wakishangilia, na sauti zimeenea kote katika mji. Hizo ndizo kelele unazosikia. 46Zaidi ya hayo, Sulemani ameketi kwenye kiti chake cha ufalme. 47Pia, maafisa wa mfalme wamekuja ili kumpongeza bwana wetu Mfalme Daudi, wakisema, ‘Mungu wako na alifanye jina la Sulemani kuwa mashuhuri kuliko lako, na kiti chake cha ufalme kiwe na ukuu kuliko chako!’ Naye mfalme akasujudu akiabudu kitandani mwake, 48akasema, ‘Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye ameruhusu macho yangu kuona mrithi kwenye kiti changu cha ufalme leo.’ ”
49Waliposikia haya, wageni wote wa Adoniya wakainuka kwa hofu na kutawanyika. 50Lakini Adoniya kwa kumwogopa Sulemani, akaenda na kushika pembe za madhabahu. 51Kisha Sulemani akaambiwa, “Adoniya anamwogopa Mfalme Sulemani na ameshikilia pembe za madhabahu. Anasema, ‘Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hatamuua mtumishi wake kwa upanga.’ ”
52Sulemani akajibu, “Akijionesha kuwa mtu muungwana, hakuna unywele wake utakaoanguka juu ya ardhi; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa.” 53Ndipo Mfalme Sulemani akawatuma watu, nao wakamshusha kutoka madhabahuni. Naye Adoniya akaja akamwinamia Mfalme Sulemani, naye Sulemani akamwambia, “Nenda nyumbani mwako.”

Iliyochaguliwa sasa

1 Wafalme 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia